Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu mwaka 2022/2023, lakini wakakosa kutokana na ukomo wa bajeti, waende vyuoni kuendelea na usajili.
Wanafunzi hao wametakiwa waende vyuoni chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amebainisha hilo jana wakati anaahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge la 12 mjini Dodoma hadi Januari 31, mwakani.
“Lengo la Rais (Samia) ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo.
“Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” alisema Majaliwa.
Uamuzi wa Rais Samia umetokana na hoja binafsi iliyoibuliwa bungeni na Mbunge wa Biharamulo, Ezra Chiwelesa aliyeliomba Bunge lijadili hoja ya wanafunzi wengi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Alisema hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2022/23, ilionesha Sh bilioni 569 zilitengwa na watoto wengi wangepata mikopo baada ya fedha kuongezeka.
Majaliwa alisema, “serikali imeyapokea kwa mazingatio makubwa maoni ya wabunge na Maazimio ya Bunge yaliyotokana na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali iliyowasilishwa bungeni Novemba 5, 2022 kuhusu kuifanyia ukaguzi wa kina Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu katika mchakato mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.”
Alifafanua kuwa, “hivyo baada ya timu hiyo kukamilisha jukumu hilo, taarifa yake itakuwa sehemu ya nyaraka muhimu kwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza Maazimio ya Bunge kuhusu ukaguzi wa ufanisi katika ugharamiaji wa elimu ya juu nchini.”
No comments:
Post a Comment