Utaratibu
mpya wa Hazina kulipa mishahara moja kwa moja kwa watumishi wa halmashauri,
umefichua ‘mchezo mchafu’ wa watumishi waliofariki na watoro kulipwa mishahara.
Akisoma
risala ya washiriki mafunzo ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti
wa washiriki hao, Ramadhani Chomolla,
alisema Serikali imepata hasara kupitia utaratibu huo.
Aliitaka
Serikali kuangalia upya mfumo wa Hazina wa kuwalipa moja kwa moja watumishi,
ili kuepusha hasara hiyo ya kulipa mshahara watumishi waliofariki, watoro na
walioacha kazi.
“Mshahara
wa Julai (mwaka huu), Hazina imewalipa moja kwa moja watumishi, hivyo watoro na
waliofariki nao wamepata mishahara, hii imeiingizia Serikali hasara na watoro
wameanza kudharau wakuu wa vituo,”
alisema Chomolla.
Hata
hivyo, akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema hilo si kosa la Hazina,
ila ni halmashauri zenyewe kwa kuwa zinawajibika kupeleka mahitaji ya mishahara
na akaunti za watumishi.
“Kama
mtumishi amefariki ndani ya mwezi ambao mshahara umelipwa sio tatizo, lakini
kama amefariki siku nyingi na amelipwa, hii inaonesha kuwa fedha hizi zingefika
kwenye halmashauri zingeliwa na wachache.
“Naamini
watu wa aina hii watakuwa wawili au watatu, ikiwa zaidi ya hapo basi
halmashauri itakuwa na matatizo. Nadhani safari hii marehemu au walioacha kazi
wamewazidi ujanja,” alisema.
Alisema
hatua ya Serikali ya kulipa mishahara moja kwa moja, ilitokana na kuwapo kwa
mabadiliko ya nyongeza za mishahara na kutaka watumishi walipwe mapema.
“Ni
nafuu ya nusu lawama kuliko malalamiko ambayo Serikali ingeyapata kama
watumishi wasingelipwa mishahara, kulikuwa na mabadiliko ya mishahara na pia
ilikuwa inakaribia Sikukuu ya Idd,”
alisema.
Akizungumzia
mafunzo hayo, Ghasia aliwataka washiriki kuhakikisha changamoto zilizojitokeza
kwenye awamu ya kwanza, hazijirudii katika utekelezaji wa awamu ya pili.
Alisema
awamu ya kwanza ilikuwa na changamoto kadhaa,
ikiwemo udhaifu katika usimamizi wa fedha, matumizi mabaya ya fedha za
miradi na kuchelewa fedha za ruzuku za uendelezaji shule.
“Tumewapa
mafunzo kwa pamoja watendaji mnaohusika katika utekelezaji wa mpango huu, hivyo
hatutegemei changamoto za awamu ya kwanza kujirudia au kutokuwa na ufanisi
katika kutekeleza miradi,” alisema.
Aidha,
Ghasia alikemea tabia ya watendaji katika baadhi ya halmashauri kusingizia
mfumo wa matumizi ya fedha kwa njia ya mtandao (EPICA), kuwa ndio chanzo cha
kukwamisha utekelezaji wa miradi.
Ghasia
alitolea mfano wa kushindwa kutumika kwa Sh milioni 897 za mwaka 2012/13 kwa
ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya
Kasulu, kwa kisingizio cha mfumo wa Epica, huku fedha hizo zikitumiwa katika
matumizi mengine.
“ Linapofika
suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Epica inakwamisha, lakini fedha za
mishahara, safari au posho Epica inafanya kazi, hali hii hatutaivumilia,”
alisema.
Washiriki
411 kutoka halmashauri na mikoa 16 walishiriki mafunzo yaliyotolewa na Wakala
wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM). Mikoa hiyo ni Ruvuma, Simiyu, Singida,
Mtwara, Lindi, Tanga, Shinyanga, Geita, Morogoro, Arusha, Manyara, Iringa,
Kilimanjaro, Dar es Salaam, Dodoma na Pwani.
Waliopata
mafunzo hayo ni maofisa elimu na ofisa mipango wa mkoa na wilaya, wahandisi na
waweka hazina wa halmashauri.
No comments:
Post a Comment