Watoto wa
Kitanzania kutoka shule za kawaida na zile za kata, wameendelea kuipa nchi
heshima kimataifa, kwa kuongoza katika mashindano ya kitaaluma.
Jana
mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Naboti iliyopo Makambako
mkoani Njombe, Neema Mtwanga (16), aliibuka mshindi wa kwanza miongoni mwa
washindani 39
katika Shindano la Utunzi wa Insha,lililoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya
kusini mwa Afrika (SADC).
Huo
ni ushindi wa pili kwa watoto wa Kitanzania kimataifa, baada ya Peter Kilave, ambaye
alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Kata ya
Tushikamane ya mjini Morogoro, kushinda tuzo ya Insha bora katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) mwaka jana.
Ushindi
wa Neema ulitangazwa jana katika mji wa kitalii wa Victoria Falls nchini
Zimbabwe, kunakofanyika mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC. Neema
alipongezwa na Rais Jakaya Kikwete, aliyepo nchini humo kuhudhuria mkutano huo.
Kutokana na ushindi
huo, Neema alitunukiwa tuzo ya ushindi huo, hundi ya dola za Marekani 1,500
ambayo ni sawa na Sh milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kushiriki
katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC. Pia, amepewa zawadi ya Ipad kwa ajili
ya matumizi yake ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Nafasi ya pili
imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe.
Nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya
Etjendlovu katika Swaziland.
Insha 39 zilipokewa
kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC, ikiwa ni insha tatu kwa kila
nchi. Insha hizo zilitoka Tanzania,
Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi,
Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini,
Swaziland, Zamibia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na
kuamua washindi wa insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na
walikutana mjini Gaborone, Botswana, mwezi Julai mwaka huu kupitia insha zote
na kutoa uamuzi wa washindi.
Akizungumza
namwandishi, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Akulasi Kyando alisema amepokea kwa
furaha ushindi huo na hasa baada ya Neema kuzingatia maelekezo waliyompa.
“Tumefurahi,
tena ameitangaza shule, tulimpa moyo kwa kuwa tunamfahamu ni mwandishi mzuri
mpaka hata nyie mmemfahamu,” alisema.
Mwalimu
Kyando alisema Neema ni mwanafunzi mwenye tabia nzuri na kwa kudhihirisha hilo,
yeye ndiye Dada Mkuu wa shule hiyo.
Kwa
mujibu wa Mwalimu Mkuu huyo, hata katika taaluma, Neema amekuwa na matokeo
mazuri na hata mtihani wa mock wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni,
alipata daraja la kwanza.
Mwandishi
alitaka kujua mazingira anayotokea Neema, ambapo mwalimu wake alisema anatoka
kijijini katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa na kuongeza: “Ni kijijini na ni
mtoto wa mkulima tu.”
Ofisa
Elimu wa Mkoa wa Njombe, Said Nyachiro, alisema ofisi yake ilipata taarifa ya
kuwepo kwa shindano hilo na kupeleka kwa wakuu wote wa shule zilizopo katika
mkoa huo.
Alisema
mbali na kusambaza taarifa hizo katika mabango, wamekuwa wakiwasihi walimu
kusaidia wanafunzi wenye uwezo, kushiriki katika mashindano hayo.
Alisema
amefurahi baada ya kupata habari za mwanafunzi kutoka Njombe, kuongoza nchi 13
za SADC.
Wanafunzi
waliopenda kushiriki katika shindano hilo, walitakiwa “Kutoa mapendekezo ya
nini kifanyike katika sekta ya elimu, ili kupunguza athari za mabadiliko ya
tabia nchi kwa vijana”.
Katika
utangulizi wa insha hiyo, mwanafunzi alitakiwa kuhakikisha anamvutia msomaji
kwa kutambulisha mada na kuanza kujadili. Msisitizo katika utangulizi, ulikuwa
kumtambulisha msomaji mada na kumuingiza katika mjadala.
Alitakiwa
kueleza namna anavyofahamu mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la joto
duniani, kwa kutoa utambulisho wa moja kwa moja katika aya moja au mbili tu.
Katika
kujadili, mwanafunzi alitakiwa kuanza kujadili mada kwa kufuata utaratibu
uliowekwa bayana, na aliruhusiwa kuweka vichwa vya habari kwa ufupi kutoka hoja
moja kwenda nyingine.
Katika
utaratibu huo wa usahishaji, wanafunzi walitakiwa kujadili kwa kuzingatia
mgawanyo wa sehemu tano muhimu za insha hiyo na waliruhusiwa kuweka vichwa vya
habari kwa ufupi, kutambulisha sehemu husika.
Sehemu
ya kwanza ya insha hiyo, ilipaswa kuelezea sababu za mabadiliko ya tabia nchi,
ilikuwa na alama kumi kati ya alama mia moja za insha nzima.
Sehemu
ya athari za ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi katika
maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ilipewa alama 20 kati ya alama mia moja za
insha hiyo.
Aidha,
sehemu ya kwanza kwa alama nyingi ni mafanikio na wapi paliposhindikana katika
utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kyoto, uliotaka nchi zenye viwanda
kupunguza utoaji wa hewa ukaa ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2005. Sehemu hiyo
ilikuwa na alama 25.
Pia
mwanafunzi alitakiwa kueleza changamoto katika kushughulikia athari za
mabadiliko ya tabia nchi na sehemu hiyo ilikuwa na alama 20.
Sehemu
ya mwisho kabla ya hitimisho, ambayo nayo imepewa alama nyingi yaani 25 kati ya
100, mwanafunzi alitakiwa kutoa ushauri nini kifanywe na sekta ya elimu katika
nchi za SADC ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wanafunzi
wote waliopenda kushiriki, walitakiwa kuwa makini na alama zilizopangwa katika
kila sehemu, hivyo wasahishaji walitarajia aya ziwe nyingi katika sehemu ambazo
zimewekewa alama nyingi.
Katika
hitimisho la insha hiyo, mwanafunzi alitakiwa kueleza kwa ufupi hoja muhimu
alizozitetea katika mjadala na alipaswa kuweka msisitizo kuhusu nini angependa
kifanywe na nchi wanachama wa SADC katika kupunguza athari za mabadiliko ya
tabia nchi katika Ukanda huo.
Wanafunzi
pia waliwekewa onyo kwa msisitizo dhidi ya atakayeiga insha kuwa ni kola la
kitaaluma. Lakini pia waliruhusiwa kuomba ushauri kutoka kwa walimu na kufanya
marejeo kutoka katika vyanzo vinavyotambulika.
No comments:
Post a Comment