Tanzania imetajwa kuongoza katika Afrika Mashariki kwa kuwa nchi yenye mitaji mikubwa ya uwekezaji. Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni matokeo ya juhudi za kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji, zinazofanywa na Serikali. Taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ya mwaka 2013, inaonesha Tanzania ilikuwa na mitaji kutoka nje yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 12.7 ikiipita Kenya iliyokuwa na dola bilioni 3.4 na Uganda dola bilioni 8.8.Kwa mujibu wa takwimu hizo, kwa mwaka 2013 pekee Tanzania ilivutia mitaji ya uwekezaji kutoka nje yenye thamani ya dola bilioni 1.9 na kuipita Kenya iliyovutia dola milioni 514 katika kipindi hicho.Akizungumzia takwimu hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Juliet Kairuki alisema: “Tanzania ina haki ya kujisifu...si kazi ndogo.” Alisema takwimu hizo ni kielelezo cha juhudi za Serikali kuweka sera nzuri za uwekezaji na hatua mbalimbali inazofanya kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na biashara yanakuwa mazuri.“Viongozi wetu, ikiwepo Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahusika na uwekezaji, wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kivutio cha uwekezaji, na haya ndio matunda yake,” alisema.Alisema katika juhudi hizo, Serikali imeweka vivutio mbalimbali vya uwekezaji ambavyo vinarahisisha biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje.“TIC inaamini kuwa kuongezeka kwa uwekezaji kutaleta ustawi wa maisha kwa Watanzania kwa kuzalisha ajira mpya, kuongeza mapato na kuleta teknolojia na ujuzi mpya,” alisema.Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Kairuki alitoa angalizo akisema kuwa pamoja na kwamba Tanzania imevutia mitaji mikubwa, bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika kushawishi kampuni kubwa za kimataifa kujenga miradi mikubwa kama viwanda hapa hapa nchini.Alifafanua kuwa bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika kubuni fursa mpya za uwekezaji kuvutia zaidi mitaji.TIC iliundwa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuratibu, kuvutia na kusaidia uwekezaji nchini na kushauri serikali kuhusu masuala ya sera za uwekezaji.Chombo hicho kinahusika na uwekezaji wenye kiwango cha chini cha mtaji cha dola 300,000 kwa wawekezaji wa nje na dola 100,000 kwa wawekezaji wa ndani.

No comments:
Post a Comment