Monday, July 7, 2014

TANAPA WAOMBA CHUO CHA UTALII KUCHANGIWA FEDHA

Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya  Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allen Kijazi ameshauri wadau wa Sekta ya Utalii kuanzisha harambee kuchangia fedha kwa ajili ya  kukisaidia Chuo cha Taifa cha Utalii,  Kampasi ya Arusha.
Alitaka hilo lifanyike kukiwezesha chuo hicho kutoa wahitimu wengi wenye taaluma ya utalii watakaoweza kupambana na soko katika Sekta ya Hoteli/Utalii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha Kijazi  aliahidi kutoa msaada wa kompyuta 10  na viti 150 kwa chuo hicho kukabili changamoto zinazowakabili wanafunzi.
Aliyasema hayo jana jijini hapa kwenye mahafali ya nne ya chuo hicho pamoja na kutunuku vyeti kwa wahitimu 79 waliomaliza masomo ya upishi na masuala ya hoteli.
Alisema Watanzania wengi wanachangia kwenye sherehe mbalimbali na kuzifanikisha hivyo  ni vyema sasa wadau wa Sekta ya Utalii na Maendeleo nao wakakutana ili kuchangia Sekta ya Utalii ambayo hivi sasa inakua na kutoa ajira kwa vijana katika nyanja mbalimbali.
“Tutaanzisha harambee ya kuchangia Sekta ya Utalii na wadau naomba mjitokeze ili kuchangia sekta hii tunataka Arusha iwe kitovu cha utalii kwani utalii upo huku na Sekta ya Hoteli na Utalii kwa hivi sasa inakua hivyo ni vyema tukaweka msukumo katika sekta hii.”
Mkurugenzi wa Mafunzo chuoni hapo, Naiman Mbise alisema chuo hicho kinakabiliwa na ukosefu wa walimu wa masuala ya chakula hivyo ni vyema Wizara ya Maliasili na Utalii ikawaongeza walimu hao na kuangalia uwezekano wa kuwajengea hosteli ili kuwaepusha wanafunzi wanaotoka mikoa mbalimbali na nchi jirani kukaa nje ya chuo.
Alisema  chuo hicho pia kinakabiliwa na changamoto ya kutumia mkaa badala ya gesi hivyo ni vyema suala hilo likaangaliwa kwa ukaribu ili chuo kiweze kutumia umeme wa nishati ya biogasi  itakayosaidia kuokoa mahitaji mbalimbali badala ya hivi sasa kutumia mkaa pekee katika kuoka mikate, keki na vitu vinginevyo.
Mwakilishi wa wazazi, Hellen Kijo- Bisimba aliwasihi wahitimu hao kuachana na kasumba ya kusubiri kuajiriwa bali watumie uzoefu walionao kuhakikisha wanatafuta soko la ajira.

No comments: