Friday, July 11, 2014

SUMAYE AFICHUA RUSHWA ZINAZOITESA TANZANIA

Waziri Mkuu mstaafu  Frederick Sumaye, ametaja aina tatu ya rushwa  zinazoitafuna nchi, ambazo ni rushwa kujikimisha haramu, rushwa ulafi na rushwa madaraka uroho.
Alisema hayo jana alipokuwa akizindua Tawi la Mwanza la Taasisi ya Tanzania Youth Development Centre (TYDC) na kufafanua kila aina ya rushwa na namna inavyoumiza Watanzania.
Katika rushwa kujikimisha haramu, Sumaye alisema wanaopokea rushwa ya namna hiyo, hujidai wanafanya hivyo ili kujikimu maisha yao bila kujali hata kama anayemdai ana hali duni kuliko yake.
“Rushwa hii huhamisha haki kutoka kwa anayestahili na kwenda kwa asiyestahili au humnyima tu huduma mwananchi anayostahili kupewa bure na kumlazimisha ainunue kwa kutoa hongo.
“Rushwa hii huumiza sana wananchi wa kawaida na ni chanzo kikubwa cha malalamiko na manung’uniko ya wananchi dhidi ya Serikali yao. Mifano ni mingi sana katika taasisi zetu na idara zetu za huduma,” alisema.
Kuhusu rushwa madaraka uroho, Sumaye alisema hutolewa kwa njia mbili; mosi katika kusaka madaraka ya utendaji ambapo mtu hutoa rushwa ili labda apandishwe cheo na inayotolewa katika kusaka madaraka ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Sumaye, rushwa za kusaka madaraka ya utendaji zipo lakini siyo kwa kiwango cha kutisha na athari zake kwa jamii zipo lakini si kubwa sana.
Alisema rushwa hiyo ya madaraka ya kisiasa ikitumika na mhusika akifanikiwa, huwa hana sababu ya kuwahudumia waliompigia kura kwa sababu katika uchaguzi kilichofanyika ni biashara, ambapo alitoa fedha na mpiga kura akamwuzia kura yake na biashara ikaishia hapo.
*Ulafi
Kuhusu rushwa ulafi, Sumaye alisema wananchi wanaweza wasiione moja kwa moja kwa sababu ni ya wakubwa wanaotoa uamuzi  wa miradi mikubwa ya Taifa, ambapo mhusika anaweza kuwekewa asilimia fulani ya gharama za mradi kama fedha zake binafsi na fedha hizo au chochote walichokubaliana, wakapeana kwa utaratibu wowote watakaokubaliana.
Alisema katika mazingira hayo, mradi husika utajengwa chini ya kiwango kwa sababu sehemu ya fedha za mradi zimeingia mfukoni mwa mtu na ili zilizobaki zitoshe, ni lazima warashie rashie mradi.
Katika rushwa ya aina hiyo, Sumaye alisema msimamizi wa mradi huo hufumbwa macho asione tena, huzibwa masikio asikie tena na hufungwa mdomo asiseme tena.

No comments: