Monday, July 14, 2014

RC AONYA WANAOHARIBU CHANZO CHA MAJI NTOMOKO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi amepiga marufuku shughuli zote zinazohatarisha chanzo cha maji cha kihistoria cha Ntomoko kinachohudumia vijiji takribani 17 vya Wilaya ya Kondoa na Chemba.
Amewataka wananchi wanaoharibu mazingira kutumia mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, kujitafakari, kufanya toba na kuacha mara moja tabia hizo sambamba na kuungana na kuwa askari kwa wengine.
Shughuli zilizopigwa marufuku ni ukataji miti, kilimo na uchungaji mifugo kwenye safu za milima ya vijiji vya Mafai, Haubi, Ntomoko na Kitongoji cha Mwisanga zinazosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuhatarisha uhai wa chanzo cha maji cha Ntomoko.
Dk Nchimbi alipiga marufuku mwishoni mwa wiki alipofanya ziara wilayani hapa kukagua miradi ya maendeleo na hali ya uhifadhi wa mzingira ambapo aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kuacha mara moja shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira.
Alisema ni muhimu kwa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha Kata ya Haubi inarudisha sifa yake ya utunzaji mazingira na kunusuru chanzo cha maji cha Ntomoko ambacho Serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni tatu kukarabati chanzo hicho na miundombinu
ya kusambazia maji kwenye vijiji hivyo 17.
Alisema chanzo hicho kiliasisiwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 1970 mbapo yeye mwenyewe alipiga kambi na kushiriki kazi ya kuchimba mitaro ya kusambaza maji vijijini.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya uhifadhi wa mazingira katika wilaya hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Isdory Mwalongo alisema uharibifu wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji imekuwa kero kubwa kwenye maeneo mengi ya Kondoa.
Mwalongo alisema uharibifu huo unajumuisha ukataji na ufyekaji miti, upasuaji wa mbao, uchomaji moto misitu, uchomaji mkaa na kilimo cha uvamizi katika misitu na vyanzo vya maji.
Alisema Halmashauri ya Wilaya imekuwa ikifanya jitihada kupambana na uharibifu wa mazingira lakini kumekuwepo na changamoto kadhaa zinazokwamisha ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika kusimamia shughuli za uhifadhi wa mazingira.

No comments: