Idadi kubwa ya wajawazito katika Tarafa ya Mwese, Halmashauri ya Wilaya ya
Mpanda mkoani Katavi, wanalazimika
kutohudhuria kliniki na kujifungulia
nyumbani, kwa madai ya kukataliwa kuhudumiwa katika kliniki ya eneo
hilo, wanapokwenda bila ya wenza wao.
Inadaiwa kuwa wanaume wengi katika Tarafa
hiyo ya Mwese, wanakataa
kuwasindikiza kliniki wenza wao kwa hofu kuwa
watalazimishwa kupima afya
zao, hususani Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Diwani
wa Viti Maalumu wa Kata ya Mwese, Theodola Kisesa alibainisha hayo wakati akichangia katika Kikao
cha Baraza la Madiwani wa
Halmshauri ya Wilaya ya Mpanda
kilichoketi juzi mjini hapa.
Akifafanua, alisema wajawazito katika
tarafa hiyo wamekuwa wakikataliwa
kupimwa afya zao na watoa huduma
katika kliniki, wanaposhindwa
kuongozana na wenza wao wa kiume
ili nao waweze kupima afya zao.
“Watoa huduma katika kliniki hii ya
Tarafa ya Mwese wanawataka
wajawazito kuandamana na
wenza wao ili nao waweze
kupima afya zao katika jitihada za kuzuia
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama na mtoto… sasa wanaume wengi
wamekuwa wanasita.
“Hivyo
baada ya kukataliwa wajawazito
wengi wamekuwa wakilazimika kujifungulia nyumbani
au kwa wakunga wa jadi ambao hawana ujuzi
wa kutosha hivyo kusababisha maisha ya mama na mtoto
ambaye hajazaliwa kuwa mashakani,
“ alisisitiza.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph
Msemwa akichangia alisisitiza kuwa
jukumu la kupimwa afya, sio la mama peke yake, bali kwa
wenza wote.
Alisema anazo
taarifa kuwa mama akipimwa na kugundulika hana maambukizi ya VVU,
mwenza wake anaamini naye yuko salama, jambo alilosisitiza
kuwa halina ukweli.
Aidha, aliagiza wajawazito wahudumiwe katika
vituo vya kutolea huduma bila ya
ubaguzi, hata kwa ambao hawakuongozana na wenza
wao.

No comments:
Post a Comment