Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ameelezea
kusikitishwa kwake na utendaji usioridhisha wa madiwani wa Halmashauri ya
Wilaya ya Monduli, akitolea mfano kushindwa kutekeleza maamuzi ya vikao vya
Baraza la Madiwani.
Miongoni mwa maamuzi ambayo hayajafanyiwa kazi
ni kuhamishia familia 53 katika shamba la Ugoro, lililokuwa linamilikiwa na mwekezaji.
Lowassa ambaye ni `mchungu’ katika suala la
uuzaji ardhi wilayani humo, aliyasema hayo juzi akiwa katika Kijiji cha Lekruko
Kata ya Nanja alikokwenda kuzindua Bwawa la Migwara, lilijengwa na Kampuni ya
Meeri, ambako alitumia fursa hiyo kuwalaumu madiwani wa Monduli kwa kufanya
kazi kwa kasi ndogo mithili ya konokono.
Bwawa hilo lililogharimu Sh milioni 870
linatarajiwa kuhifadhi maji yenye lita za ujazo 218,381,000.
Aidha, kukamilika kwa bwawa hili kutaongeza
kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji Monduli kutoka asilimia 53.85 Desemba
mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 58.9 mwezi huu.
“Madiwani mnachelewa kutekeleza maamuzi
yanayochukuliwa, angalia tangu tulipokubaliana kuchukua shamba la mwekezaji wa
Ugoro pale Makuyuni mpaka leo hakuna kilichofanyika.
“Tulipitisha azimio kwamba familia 53
zinazoishi maeneo ya Jeshi la Wananchi zihamie katika shamba hilo, lakini hadi
leo hii hakuna kilichofanyika. Madiwani mnafanya uamuzi pole pole kama
konokono,” alisema Lowassa.
Katika harakati hizo za kupigania ardhi
isiendelee kununuliwa na watu wachache kisha kutotumiwa, Lowassa alisema
haiingii akilini kuona Halmashauri imechukua baadhi ya mashamba kwa ajili ya
manufaa ya wananchi, kisha haiyaendelezi au kushindwa kupangia matumizi
mengine.
Akizungumza kuhusu suala la maji wilayani
Monduli, alisema maji wilayani humo, yameendelea kuwa changamoto na hasa katika
namna ya kuyapata licha ya kuchimba visima.
“Ndugu
zangu kuna maneno yanaendelea huko nje, eti maji Monduli ni machafu, naomba
niwaambie haya ndio aina ya maji yanayopatikana Monduli tangu wakati wa Utawala
Hayati Edward Sokoine, aliyewahi kuleta
watu wa kuchimba visima vya maji hakufanikiwa.
“Nimejaribu pia hata mimi kuendelea kutafuta
maji ya chini bado hakuna maji chini ya ardhi ndio maana tukaamua kuja na njia
mbadala ya kujenga mabwawa ili tuvune maji ya mvua, hao wanaosema tunaowamba
walete nguvu zao nao kujaribu kuchimba badala ya kusema tu,” alisema Lowassa.

No comments:
Post a Comment