Saturday, June 21, 2014

SABASABA 2014 KUUNGANISHA UZALISHAJI NA MASOKO

Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Maonesho ya Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika kwa siku kumi kuanzia Juni 28, mwaka huu katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius  Nyerere, Dar es Salaam yanatarajiwa kuongozwa na kaulimbiu ya `Tunaunganisha Uzalishaji na Masoko’.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi  ya Maendeleo ya Biashara nchini (TanTrade), Jacqueline Mneney Maleko, kaulimbiu hiyo imechaguliwa kutumika kuonesha uhusiano uliopo kati ya Uzalishaji na Masoko  na umuhimu wa mnyororo wa uzalishaji, ambao ni chimbuko la upatikanaji wa bidhaa zenye ushindani katika soko. 
Alisema kwa mwaka huu, TanTrade imetenga eneo kubwa zaidi kwa ajili ya wazalishaji wa ndani ya nchi.
Alibainisha kuwa maeneo yatakayotumiwa na wazalishaji hao kuwa ni Jengo Namba C.19 na eneo la wazi, lililo nyuma ya ofisi za Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Uwezeshaji kwa ajili ya bidhaa za kilimo na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania.
Kuhusu ushiriki wa mataifa mengine katika maonesho hayo, alifafanua kuwa tayari nchi 31 zimethibitisha kushiriki, zikiwemo Afrika Kusini, Jamhuri ya Czech, China, Ghana, Indonesia, India, Iran, Finland, Ugiriki, Italia, Japan, Jordan,
Kenya, Korea Kusini, Malaysia, Marekani, Misri na Ujerumani. Nyingine ni Nigeria, Pakistan, Rwanda, Saudi Arabia, Singapore, Sudan, Syria, Uganda, Uingereza, Burundi, Sweden, Vietnam na Zimbabwe.  Jumla ya washiriki waliothibitisha kushiriki kutoka ndani ya nchi ni 1,700.

No comments: