Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imekamilisha rasimu ya miswada mitatu ya
sheria za usalama wa mtandao ili kudhibiti uhalifu katika mitandao.
Akiwasilisha
makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, Waziri Profesa Makame Mbarawa alitaja
miswada hiyo kuwa ni Sheria ya Usalama wa Mtandao, Sheria ya kulinda Taarifa
Binafsi, Sheria Miamala ya Kielektroniki na sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa
Mtandao na Kompyuta.
Alisema rasimu
hizo zimewasilishwa kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali ili ziweze kuandaliwa kwa
mujibu wa taratibu za uandishi wa sharia.
Pia
alisema wizara hiyo imetengeneza kanuni
mpya zinazosimamia mawasiliano kupitia mitandao ya simu ambao ulianza kazi
mwezi Oktoba mwaka jana kwa kampuni za nje kutakiwa kulipa senti 25 za Marekani
kwa kila dakika moja ya mazungumzo ya simu zinazoingia nchini kutoka nje.
Alisema katika
kanuni hiyo mpya, imeweka mgawanyo wa mapato hayo ya senti 25 ambapo serikali
kupitia hazina inapata senti saba, watoa huduma wanapata senti 13 na senti tano
ni kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ikiwa ni pamoja na kumlipa mwekezaji wa
mitambo huo.
“Hadi kufikia
mwezi Januari mwaka huu, mfumo huu umeweza kuingizia Serikali jumla ya shilingi
bilioni 6.8, mtambo huo pia unaratibu dakika za maongezi kwa simu za kimataifa
na kufuatilia udanganyifu kwa simu zinazoingia nchini ambapo mpaka sasa
udanganyifu umepungua kutoka asilimia 60 kabla ya mdandao huo kufungwa hadi
asilimia mbili,” alisema.
Alisema katika
kuweka mazingira mazuri ya kukuza sekta ya mawasiliano na kuimarisha uratibu
pia wizara imekamilisha uandaaji wa rasimu ya sera mpya iliyohuishwa na rasimu
ya mkakati wa utekelezaji wa sera mpya.
Akiwasilisha
maoni ya kamati ya Miundombinu, Makamu Mwenyekiti Juma Kapuya alishauri Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza nguvu katika kusimamia usalama wa
mawasiliano ya mtandao wa kompyuta kwa hali ilivyo sasa kumekithiri wizi na
utapeli katika mitandao.

No comments:
Post a Comment