Sunday, June 22, 2014

KAMPUNI 450 ZA NJE KUSHIRIKI MAONESHO YA SABASABA

Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanatarajiwa kuwa mazuri zaidi, baada ya kampuni zaidi ya 450 za nje ya nchi, kuthibitisha kushiriki.
Mbali na kampuni hizo za nje ya nchi, kampuni za Tanzania 1,700 nazo zimethibisha kushiriki katika maonesho hayo, huku wizara na taasisi za umma zilizothibitisha kushiriki ni 61. Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania(TanTrade), Anna Bulongo, wakati akizungumzia maandalizi ya maonesho hayo. Alisisitiza kuwa maandalizi yamefikia katika hatua nzuri zaidi.
"Suala la udhibiti wa uhalifu ndani na nje ya uwanja, ulinzi umeimarishwa zaidi,  kutakuwa na CCTV kamera kwa ajili ya kuwabaini wahalifu," alisema. 
Alitaka washiriki wa maonesho hayo, ambao bado hawajamaliza kulipa ada za ushiriki, wafanye hivyo haraka ili waweze kupatiwa vitambulisho maalumu.
Maonesho hayo yanatarajiwa kuanza Juni 28 mpaka Julai 8 mwaka huu katika Viwanja vya maonesho vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa. 
Bulongo aliwataka Watanzania kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kutangaza zaidi biashara zao ili ziweze kupata soko kwani ni muda mzuri wa wao kufanya hivyo.

No comments: