Saturday, June 21, 2014

JESHI LA MAGEREZA KUANZA KUCHIMBA MADINI


Katika kukabiliana na tatizo la ufinyu wa bajeti katika Jeshi la Magereza na kuipunguzia mzigo Serikali, jeshi hilo linakusudia kuanza kuchimba madini ili lijitegemee, baada ya utafiti wa jeshi hilo kubaini baadhi ya maeneo inayoyamiliki yanaweza kuwa na aina mbalimbali za madini.
Tayari jeshi hilo limeshapata leseni 102 za uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali nchini ili liweze kupata fedha za kujiendesha.
Hayo yalisemwa jana na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Minja katika hotuba yake aliyoisoma mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Magereza nchini yaliyohudhuriwa pia na wakuu wa vyombo vya ulinzi na wastaafu wengine wa jeshi hilo.
Alisema jeshi lake linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo ufinyu wa bajeti, miundombinu ya magereza, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri na mawasiliano, vitendea kazi, ukosefu wa pembejeo pamoja na msongamano magerezani.
“Katika kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa bajeti, Jeshi la Magereza limefanya jitihada mbalimbali ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu, tumefanyia utafiti maeneo yetu na tayari tumekwisha pata leseni 102 za uchimbaji madini, sasa tunatafuta wawekezaji,” alisema Kamishna Minja.
Alisema leseni hizo ni za uchimbaji wa madini ya ujenzi kama chokaa, mawe, kokoto, mchanga na moram katika maeneo mbalimbali ya Magereza nchini. Aliongeza kuwa, jeshi hilo linaendelea kuomba leseni nyingine katika maeneo yanayoonekana kuwa na madini.
Mbali na hilo Kamishna Minja alisema Magereza imeingia pia ubia na Mfuko wa Pensheni wa Akiba ya Wafanyakazi (GEPF) kwa ajili ya uwekezaji wa miradi mbalimbali kwa ubia katika maeneo ya Magereza ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majumba makubwa ya biashara (Mall).
Alisema katika kukabiliana na tatizo la makazi ya watumishi, Jeshi linafanya jitihada za kuhamasisha ujenzi wa nyumba za kujitolea kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo husika.
“Jitihada hizi zimeonesha mafanikio makubwa kwani hadi sasa nyumba nyingi za kujitolea zimejengwa na kukamilika na nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi na pia tunaendelea na ukarabati wa nyumba za zamani,” alisema Kamishna Minja.
Aidha alisema wamefungua kiwanda cha ushonaji katika Gereza la Butimba mkoani Mwanza kwa lengo la kupunguza wingi wa kazi za ushonaji uliokuwepo kiwanda cha Ukonga ambapo ni fursa nzuri kwa wafungwa pia kujifunza shughuli za ushonaji kama sehemu ya urekebishaji.
Alisema kiwanda kingine kimefunguliwa Ruanda, Mbeya na kiwanda cha samani kiko mbioni kukamilika katika Gereza la Lilungu mkoani Mtwara.
Alisema Jeshi hilo katika kuhakikisha wanaimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, wameingia ubia na baadhi ya kampuni za ndani na nje ili kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji.
“Hii ni jitihada za kulifanya Jeshi la Magereza linakuwa la kisasa katika utekelezaji wa majukumu yake na pia kushukuru taasisi zisizo za kiserikali kuona maeneo ya shughuli mbalimbali tushirikiane, kutushauri na mapendekezo ili kuboresha utendaji kazi,” alisema Kamishna Minja.
Awali Waziri Chikawe alifungua duka la bidhaa zisizotozwa ushuru katika Magereza ya Keko jijini Dar es Salaam ambapo Kamishna Minja alisema duka hilo ni moja kati ya maduka kadhaa yaliyopo mikoa mbalimbali na kwamba Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na wabia wengine wataendelea kufungua maduka mengine.

No comments: