Sunday, April 13, 2014

UJENZI WA NYUMBA MRADI WA GESI WAKAMILIKA KWA ASILIMIA 82

Ujenzi wa nyumba za kudumu kwa ajili ya makazi ya wafanyakazi wa mradi wa gesi asilia kwenye   eneo la Madimba, Mtwara Vijijini, umekamilika kwa asilimia 82, wakati wa nyumba za Songosongo wilayani Kilwa ukiwa umekamilika kwa hatua ya msingi na kuta.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Maliki Munisi alisema nyumba zilizopo kwenye eneo la Songosongo zimekamilika kwa asilimia 58.
Katika hatua nyingine, Munisi alisema usafishaji wa njia ya kulaza bomba unaendelea na kwamba, kilometa 499.12 kati ya kilometa 517 zinazohitajika, zimekamilika.
Kwa maelezo yake, kazi ya kuunganisha mabomba inaendelea kama ilivyopangwa, ambapo, hadi sasa, mabomba ya kilometa 363 yamekwishaunganishwa.
Akizungumzia uchimbaji wa njia ya kulaza bomba katika maeneo ya Dar es Salaam, Mkuranga, Bungu, Kiwawa, Nangurukuru na Mtwara, Munisi alisema, kilometa 231 zimekwishachimbwa.
 Vilevile,  ujenzi wa kituo cha kupokea gesi katika eneo la Somanga Fungu na Kinyerezi nao umeanza sambamba na ujenzi wa bomba la baharini katika eneo la Somanga kuelekea Songo Songo ambapo, kilometa 25 zimekamilika.

No comments: