Sunday, April 13, 2014

NAPE AMSHUKIA MNYIKA BUNGE LA KATIBA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amemwashia moto mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema) pamoja na wabunge wengine wa upinzani bungeni, kwa kitendo  cha kudai hati za muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amekiita kitendo sawa na mtoto kudai cheti cha ndoa cha wazazi wake.
Kiongozi huyo wa CCM aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Manyovu wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, wakati wa ziara ya Katibu mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana mkoani humo ya kukagua utekelezaji wa Ilani na kuimarisha chama hicho.
Nape ni kama alikuwa akimjibu Mnyika msemaji wa Chadema na Ukawa alipoomba mwongozo juzi bungeni wa kutaka kikao cha Bunge hilo kilichokuwa kikiendelea kiahirishwe mpaka watatue unaoitwa mgogoro wa hati za Muungano.
Alisema mwenendo wa vyama vya upinzani nchini unatia shaka, hasa vile vilivyopata fursa ya kuingiza watu kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa kuanzisha Ukawa, hali ambayo ni dalili tosha kuwa vimekata tamaa na kuamua kuanzisha chombo hicho ili kuanzisha vurugu kukwamisha mchakato wa Katiba mpya.
Kuhusu tabia ya vyama hivyo ya kukimbilia maandamano pale vinapoona hoja zao zimepuuzwa, Nape  alisema safari hii vikiamua kukimbilia barabara hata chama hicho nacho kitafanya hivyo ili kueleza ukweli.
Akizungumzia suala la vyama hivyo kutaka Bunge liahirishwe hadi pale itakapowasilishwa hati ya muungano, Nape alisema wapinzani hao wameanzisha hoja hiyo baada ya kuona hoja yao ya kutaka muungano uvunjwe kupitia Serikali tatu imekufa rasmi baada ya hotuba nzuri ya Rais Jakaya Kikwete ya kufungua Bunge hilo hilo.

No comments: