Friday, April 11, 2014

BILIONEA BUFFETT ACHANGIA SHILINGI BILIONI 3.8 VITA DHIDI YA UJANGILI

Bilionea wa Kimarekani Howard G. Buffett  kupitia taasisi yake ametoa msaada zaidi  wa kukabiliana na ujangili, ikiwemo helikopta pamoja na kusomesha marubani.

Msaada huo una thamani ya shilingi bilioni 3.8.
Awali taasisi hiyo ilinunua helikopta moja aina ya R44 na sasa itakodisha nyingine ya  aina hiyo na hivyo kuwezesha kuwapo kwa helikopta nne angani kutokana na  serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kununua moja na nyingine inanunuliwa na Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, ufadhili wa bilionea huyo kwa sasa umefikia Sh 8,577,060,000 ikiwemo mafunzo ya marubani, kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi 300, jiko la kisasa na karakana.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri Lazaro Nyalandu inaeleza kuwa pia kuna ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua, ununuzi wa mabasi aina ya Scania mawili na malori aina ya Scania mawili pamoja na mafunzo na mradi wa kuhifadhi Duma.
Alisema helikopta iliyonunuliwa  ni kwa ajili Pori la Akiba la Selous ambayo inatarajiwa kuwasili nchini ndani ya kipindi cha miezi 6 kuanzia sasa.
Alisema helikopta iliyokodiwa na taasisi hiyo, itafanya ulinzi  wa doria chini ya Mkurugenzi wa Wanyama pori katika Pori la Akiba la Selous kuanzia katikati ya mwezi Mei, mwaka huu wakati zikisubiri helikopta zilizoagizwa kutoka viwandani nchini Marekani.
“Helikopta hii itatumika kwa miezi sita  kuanzia siku itakayowasili nchini, Taasisi hii  itagharimia gharama za uendeshaji, ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za kuikodi ndege, marubani na mafuta, huku Wizara ikigharamia malazi na chakula cha marubani hao wakiwa katika shughuliza doria hapa nchini,” alisema.
Aidha taasisi hiyo ikishirikiana na Wizara imepata wataalamu elekezi wawili, watakaotoa ushauri wa kitaalamu katika maeneo ya Pori la Akiba la Selous na Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori – Pasiansi kwa muda wamiezi 6 kwa gharama zake huku ikigharamia  malazi na usafiri wakiwa nchini.
Nyalandu alisema Serikali kupitia Tume ya ajira imetangaza nafasi za ajira 450 kwa askari wawanyamapori, ikiwa ni sehemu ya jumla ya askari 950 ambao wanategemea kuajiriwa  kwa mwaka huu wa fedha.
Pia Wizara itakipatia Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori – Pasiansi silaha 25, aina ya AK47 kwa ajili ya kuimarisha mafunzo kwa wakufunzi.

No comments: