Dk Ali Mohammed Shein. |
Alisema katika Mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya makubaliano yalifanyika baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hivyo ni serikali mbili ambazo zilikubaliana na si zaidi.
Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein katika uzinduzi wa Sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambazo kilele chake ni Aprili 26 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Dk Shein imekuja wakati tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakiweka wazi misimamo yao kuwa ni serikali mbili.
"Katiba ya Jamhuri imefanyiwa marekebisho mara tano kama siyo saba, wakati tunafanya marekebisho ya Katiba ya Zanzibar tulikubaliana iwe ni serikali mbili.
"Mchakato huu wa Katiba mpya unaoendelea ulikubaliwa na serikali mbili, kwa hiyo yale yote yanayoendelea mpaka hivi leo, serikali mbili tumekubaliana," alisisitiza Dk Shein.
Akizungumzia kuhusiana na Muungano, Dk Shein alisema hakuna anayeweza kuutengua Muungano huo kwa namna yoyote kutokana na kuwa ni wa kihistoria na ulianzishwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla.
"Kuna undugu wa damu kabisa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ambao hatuwezi kuutenganisha wala kuukataa, hivyo ni lazima tuhakikishe Muungano unadumishwa daima," alisema Dk Shein.
Alisema muungano ulifanywa na wananchi wenyewe chini ya marais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na wa Zanzibar Abeid Amani Karume, kuwa umedumu kutokana na dhamira za dhati walizokuwa nazo viongozi hao.
"Muungano una manufaa makubwa kwa watu wa pande zote mbili ambayo ni ya kijamii na kiuchumi na kufanya mustakabali mzuri kwa taifa kiujumla. Pia Muungano umekuwa imara zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma," alisema.
Alisema hali ilipofikia hivi sasa ni pazuri kwa mwananchi mmoja mmoja kutoa maoni yake, makundi na hata viongozi walitoa maoni, hivyo anaamini wajumbe wa Bunge hilo Maalumu la Katiba watazingatia maoni na matakwa ya Watanzania ya Katiba wanayoitaka.
"Wao wakimaliza watuletee sisi wenyewe na sisi tutapendekeza Katiba gani tunayoitaka, kwa sababu ni yetu wenyewe," alisema.
No comments:
Post a Comment