ATUHUMIWA KUKUTWA UCHI AKIFUKUA KABURI LA MWANAMKE...

Mkazi wa Kijiji cha Ikola katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda  Mkoa wa Katavi, Richard Clavery ( 34 ) amefikishwa  mahakamani  kwa tuhuma ya  kufukua  kaburi la mwanamke, aliyekufa na kuzikwa  kaburini humo.

Mtu huyo anatuhumiwa kukutwa na waombolezaji,  akiwa  amevua nguo zake zote  na kuzitundika  juu  ya  msalaba,  uliosimikwa  kaburini hapo.
Mwendesha Mashitaka, Godfrey Luzabila alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda,  Chiganga Ntengwa,  Februari   25 mwaka huu kuwa  mshtakiwa   alitenda kosa hilo  Februari  18 mwaka huu saa nne usiku nyumbani kwa  dada wa marehemu,  Lenada  Sakafu  katika kijiji cha Ikola .
Luzabila  alidai usiku wa tukio hilo,  mtuhumiwa alifika nyumbani kwa Lenada  Sakafu na kufukua  maiti ya mdogo wa Lenada, Tabu Omera  aliyekuwa  amezikwa  kaburini   siku tatu kabla ya tukio  hilo. Kaburi  alimozikwa marehemu,  lilikuwa  katika eneo  la  nyumba ya Lenada.
Alidai usiku huo, Lenada  akiwa nyumbani  hapo pamoja na  waombolezaji,  wakiwemo  majirani na ndugu,  ghafla alitokea  mtoto wa Lenada,  aitwaye  Brandina ambaye aliwaeleza  kuwa ameona mtu nje ya nyumba  yao  akifukua kaburi la Tabu.
Waombolezaji hao papo hapo  walitoka nje   na kumkuta  Clavery   akifukua kaburi  hilo, huku akiwa  amevua nguo zake zote  na kuzitundika  juu  ya  msalaba  uliosimikwa  kaburini hapo.
Walipomsemesha mtuhumiwa huyo, alijifanya amepandisha majini na kujaribu kutoroka. 
Mtuhumiwa  alikana shitaka  hilo. Hakimu  Ntengwa  alilazimika kuahirisha  shauri  hilo  hadi Machi 6 , mwaka huu litakapotajwa  tena.
Hakimu aliamuru  mshtakiwa  arejeshwe  rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo alitakiwa adhaminiwe na mtu mmoja kwa kiasi cha Sh  milioni moja .

No comments: