WATOTO WA DARASA LA SABA KIZIMBANI KWA MADAI YA KUOANA RUKWA...

Mwanafunzi aliyehitimu Darasa la Saba mwaka jana, jina tunalo amefikishwa  katika Mahakama ya  Hakimu wa Wilaya ya  Nkasi mkoani Rukwa, kwa madai ya kumuoa  msichana  waliyekuwa  wakisoma  naye darasa moja  mwenye  umri  wa miaka  15.

Binti huyo alifanikiwa kupata nafasi ya kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Chala  wilayani Nkasi, lakini ameshindwa kujiunga kwa kuwa ni mke wa mtu.
Wawili hao walikuwa wakisoma Shule ya Msingi Kacheche kijijini Kacheche  wilayani Nkasi.
Mshtakiwa ambaye  kwa sasa  ni  mkulima  katika  kijiji  cha Kacheche  alifikishwa mahakamani  hapo  jana mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Ibrahim Mgalamalira  ambapo  alikana  shtaka  hilo.
Mtuhumiwa alidai kuwa  anafahamu  kuwa amemaliza  elimu ya msingi,  lakini hakuwa na taarifa  kama  alikuwa amechaguliwa kujiunga na  elimu  ya sekondari  mapema mwaka huu.
Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa  mtuhumiwa alimuoa  msichana huyo, Februari 24, mwaka huu na kuishi  naye nyumba moja kijijini  Kacheche  kama mume na mke  kwa  siku sita  hadi alipotiwa nguvuni Machi 3, mwaka huu.
"Msichana huyu bado ni mwanafunzi kwa kuwa  alichaguliwa  kujiunga Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Chala wilayani hapa lakini  ameshindwa kuendelea na masomo kwa  kuwa  alikuwa ameolewa na mtuhumiwa ambaye sasa amemkatisha masomo yake," alidai mahakamani hapo Mwendesha Mashtaka.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa  alipohojiwa kwa mara ya kwanza kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, alikiri  kumuoa  msichana  huyo   kwa kuwa  alifahamu  kuwa  ameshamaliza  darasa la saba  mwaka jana.
Hakimu Mgalamalira  aliamuru  mshtakiwa  arudishwe  rumande baada ya kushindwa  kutimiza masharti ya  dhamana  ambayo  alimtaka  awe na  wadhamini wawili  wenye mali  zisizoweza kuhamishika  zenye thamani  isiyopungua  Sh  milioni  moja.
Shauri  hilo  limeahirishwa  hadi Machi 26, mwaka huu  litakapotajwa  tena.

No comments: