Samuel Sitta akila kiapo kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba jana. |
Sitta ameanza kazi huku wajumbe wengi wakiwa na imani naye kuwa ataliendesha Bunge hilo lenye mchanganyiko wa watu kwa haki na kwa viwango na kasi; lakini mwisho wake ni kuwapatia watanzania katiba nzuri wanayoitarajia.
Akizungumza jana baada ya kupishwa kiti hicho na mwenyekiti wa muda Pandu Ameir Kificho, Sitta alimsifu mwenyekiti huyo wa muda kwa vile aliendesha bunge hilo bila kanuni, hivyo kulifanya kutawaliwa na vituko vya wabunge kupiga kelele
“Sasa tuna kanuni mambo ya kupiga kelele na kuwasha kipaza sauti bila kuruhusiwa, mtanilaumu bure, tusilaumiane, nitakuwa ndio natimiza wajibu wangu,” alisema Sitta.
Mwenyekiti huyo alisema Kificho alitumia busara, hekima na ustahimilivu mkubwa kuliongoza Bunge hilo ambalo halikuwa na kanuni, “Nina kitu cha kujifunza kwa mzee huyu kwa namna alivyoliendesha bunge hili kwa wiki tatu bila kuwa na kanuni.”
Alisema kitu kikubwa ambacho Kificho atakumbukwa ni kuliongoza Bunge hilo; lakini kwa kuteua kamati nzuri ya kanuni ambayo ilifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na akaahidi kuwatumia wajumbe hao katika kamati zingine zitakazoundwa.
Katika ahadi yake baada ya kuchaguliwa, Sitta aliahidi kuhakikisha wanamaliza vikao vya Bunge kwa muda uliowekwa na sheria ili wananchi wasiwaone kama wajumbe hao ni waroho wa posho.
Mara tu baada ya kuanza kazi, Sitta aliamuru siku tatu kuanzia jana jioni hadi kesho Jumapili zitumike kwa wajumbe kuapa ili Jumatatu kazi kubwa ianze kwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha rasimu bungeni hapo.
“Tunatarajia kuwa kati ya Jumanne na Jumatano, Rais atakuja kulizindua Bunge hili,” alisema Sitta na kuongeza kuwa ameamua kuwa siku tatu kabla ya wajumbe kwenda kwenye kamati wapate muda wa kuwa na mjadala mpana kwa wajumbe wote wa kujadili mambo ya jumla yaliyoko kwenye rasimu hiyo.
Kwa upande wake Kificho aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa wavumilivu na kutumia hekima na busara kwa kutoa hoja zenye mashiko zisizowagawa watanzania katika kupata Katiba mpya.
Kificho alitoa nasaha hizo wakati akikabidhi uenyekiti kwa Mwenyekiti wa kudumu, Samuel Sitta ambapo aliwataka wajumbe hao kutotoa hoja za kuwagawa watanzania kikabila, kikanda, kidini na kijinsia.
“Kazi ya kutengeneza kanuni haikuwa rahisi kwa sababu kila mmoja alikuwa na maoni na msimamo wake na kazi ya sasa ya kupata katiba japo kutakuwa na muongozo wa kanuni itakuwa ngumu kama tulivyoona hapo nyuma,” alisema Kificho aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo Februari 18 na kuongeza: “Kinachotakiwa kwenye bunge hili ni uvumilivu na kuweka mbele maslahi ya taifa na si binafsi.
Wajumbe tumieni hekima na busara tupate katiba ambayo wananchi wanaisubiri kwa muda mrefu na kutakapotokea vikwazo tumalize kwa busara”.
Awali Katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad alimwapisha Sitta na makamu mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan na baadaye wajumbe kuapishwa ambapo alianza Kificho na kufuatiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na kufuatiwa na wajumbe wenye mahitaji maalumu.
Baada ya wajumbe wenye ulemavu kuapa walifuata mawaziri wa serikali zote mbili ili kuwapa fursa ya kesho kuondoka kwenda ofisini kwa ajili ya kuendelea na vikao vya maandalizi ya bajeti.
Baada ya hapo watafuatia wajumbe wengine ambao wataapa kwa kuafuta alfabeti zao kuanzia A hadi Z bila kujali nyadhifa zao.
No comments:
Post a Comment