Sunday, March 23, 2014

WANAOISHI JIRANI NA DAMPO PUGU WATAKIWA KUHAMA BILA FIDIA...

Kazi ya usafi ikiendelea kwenye dampo la Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam.
Wiki moja baada ya kuandikwa habari kuhusu hatari ya kupata magonjwa, ikiwemo kipindupindu inayowakabili wakazi wanaoishi karibu na dampo la Pugu Kinyamwezi na hatua ya kula kwenye chandarua walioianzisha kupunguza kero ya inzi, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam umezungumzia hali hiyo.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe amekiri kuwepo kwa tatizo la hatari ya magonjwa kwa wakazi hao, lakini amesema wakazi hao ni wavamizi wa eneo la kutupa takataka kwa kuwa walilikuta dampo wakati wakijenga eneo hilo hivyo wanapaswa kuondoka.
Alisema kutokana na kuvamia eneo hilo, adha wanazopata, wamejitakia wenyewe na kuwaeleza kuwa dawa ya kumaliza adha hizo ni kuondoka kama walivyoelekezwa na Serikali mara nyingi kupitia viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohammed Gharib Bilal.
"Wale ni wavamizi wa eneo la kutupa taka, dawa ya mvamizi si kulalamika kwamba yupo hatarini kupata magonjwa, ni kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuondoka eneo hilo, serikali ilishawataka mara nyingi waondoke lakini ndio tabia zetu wananchi, hawataki kuchukua hatua hiyo," alisema Kabwe alipozungumza na gazeti hili Ijumaa.
Alipoulizwa muda waliopewa wakazi hao kuondoka, Kabwe alisema serikali kwa kutambua kuwa wale ni wanadamu kama wengine, wamepewa muda mrefu wa kuondoka taratibu na kutaka wengine wasiendelee kujenga eneo hilo lakini bado hakuna waliochukua hatua hiyo.
Kabwe alisema masuala ya siasa pia yanaingilia suala hilo, jambo linaloweka ugumu kuchukua hatua na kuongeza kuwa yanayoendelea Pugu ni kama yaliyotokea Jangwani ambako pamoja na wakazi hao kukumbwa na mafuriko na hata wengine kupoteza maisha, waling'ang'ania kuishi eneo hilo pamoja na kutengewa eneo la Mabwepande, Kinondoni jijini humo.
Hata hivyo, Kabwe alipoulizwa kwanini wakazi hao wa dampo la Pugu Kinyamwezi lililopo wilayani Ilala wasitengewe na wao eneo, alisema wakazi wa Jangwani kupewa Mabwepande ilikuwa ni huruma ya Serikali na kueleza kwamba, si kila wakati Serikali itafanya huruma kama huo.
Kuhusu hali ya inzi na miundombinu mibovu ya dampo hilo, Kabwe alisema kwa wiki mbili sasa wamekuwa wakipiga dawa na hata siku alipozungumza na mwandishi, Ijumaa iliyopita, walipiga dawa.
Akizungumzia mpango wa kulifanya dampo hilo kuwa la kisasa, Kabwe alikiri kweli kuwa miundombinu ya dampo hilo haiko vizuri na kueleza kuwa, mpango wa Serikali ni kuliboresha unaendelea. Hata hivyo hakutaka kueleza hatua ilikofikia zaidi ya kudai mchakato uanendelea.
Miongoni mwa malalamiko ya wakazi hao ni ahadi ya serikali kuwa dampo hilo lingekuwa la kisasa, likizungushiwa ukuta, kuwekewa dawa ya kuzuia madhara kwa binadamu. Tofauti na hayo, dampo hilo liko wazi, lililojaa nzi na wadudu wengine wa hatari, na mvua zinaponyesha, maji machafu hutiririka kwenye makazi ya watu.
Hivi karibuni mwandishi alifika katika dampo hilo na kubaini kuwa, wakazi waishio karibu na eneo hilo katika harakati za kujikinga na maradhi na usumbufu wanaoupata wa nzi majumbani, wamegundua mbinu mpya za kukabiliana na tatizo hilo na sasa familia zinakula chakula ndani ya vyandarua.
Familia hizo hulazimika kufunga chandarua ama sebuleni au barazani na baba, mama, watoto na wanafamilia wengine huingia ndani yake na kuzuia vizuri mianya ya nzi kuingia kwa kuweka mawe ama mbao na kisha hupata ahueni ya kula bila kuandamwa na nzi.
Hata hivyo, pamoja na ugunduzi huo uliotoa nafuu kwa kuwapunguzia maradhi, hali za afya kwao bado ni tete kutokana na harufu kali ya kemikali na taka zinazotupwa katika dampo hilo pamoja na hatari ya kupata saratani kutokana na moshi unaofuka mara kwa mara.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na gazeti hili katika makazi yao umbali wa kutengwa na barabara inayoingiza magari yanayotupa taka eneo hilo, walilalamikia hali hiyo na kueleza kuwa wameamua kugundua mbinu hiyo ili kunusuru afya zao.
Maua Hamis (22), mkazi wa Mtaa wa Kichangani Majohe, alisema watoto katika familia wamekuwa wakiugua vifua, matumbo ya kuhara, mafua na malaria kila kukicha kutokana na madhara ya dampo hilo na familia takribani zote, sasa wanalazimika kununua vyandarua zaidi ya viwili kwa ajili ya matumizi hayo.
"Hapa kwetu 'neti' (chandarua) hazina kazi ya kuzuia mbu tu usiku au mchana, bali tunazo zaidi ya mbili na familia nyingi tunazitumia kwa chakula pia, tunazifunga kwa kamba ama misumari ukutani sebuleni ama barazani na tunaweka mawe, vipande vya miti au mbao kwa chini ili nzi wasiingie kisha tunaingia wote haraka haraka na kuanza kula tukiwa ndani ya neti," alisema Maua.
Alisema mara zote wanapotaka kula iwe chai, mlo wa mchana ama usiku wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa jambo la ajabu ni kwamba nzi hao hawalali hata usiku ni wasumbufu kama wanavyofanya mchana.
Mwandishi akiwa eneo la tukio, alishuhudia wingi wa nzi hao katika bustani za mboga katika makazi ya watu, kwenye magudulia ya maji, ukutani na walikuwa wakitua na kuruka kwa wingi kwa watu, akiwemo mwandishi wa habari hizi. Awali waandishi walipofika eneo hilo na kuvuta hewa, walianza kuumwa matumbo na vichwa.
Watoto walionekana pembezoni mwa dampo wakicheza huku nzi wakiwa midomoni, puani na maeneo mengine ya mwili, maji machafu kutoka katika dampo yakiwa yanapita na kuingia katika makazi yao huku watoto hao wakicheza kwenye maji hayo bila viatu. Baadhi ya watu walionekana katikati ya dampo wakiokota vyuma chakavu, chupa na vifaa  vingine bila vifaa vya kinga.
Moses Lucas, mkazi wa eneo hilo alidai hali za afya kwa wakazi wa eneo hilo ni tete kutokana na mazingira yaliyopo hasa nyakati hizi za mvua na kuongeza kuwa, japo wanakula kwenye chandarua lakini watoto wanacheza kwenye maji machafu kutoka katika dampo hilo.
Lucas alisema kumeundwa kamati ya wananchi kushughulikia kero hizo, lakini alidai serikali imekuwa ikiwapiga danadana katika kushughulikia kero hizo ikiwemo kuboresha dampo.
Baadhi ya watoto waliozungumza na mwandishi, Rashid Abdallah (12) na Bariki Massawe (11) walisema kwa nyakati tofauti kuwa wanalazimika kufukuza nzi ndani kwa muda wa nusu saa kabla ya kuweka neti na kula chakula, pia moshi, harufu na maji machafu yanahatarisha afya zao.

No comments: