HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21
MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa
Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa
Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa
Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa
Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Othman Makungu, Jaji Mkuu wa
Zanzibar;
Viongozi
Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni
waalikwa;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa
kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la
Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na
Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya
kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa
mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa
kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo
tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini
yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili,
ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote
wa Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba
mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo
yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia
nchi yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika
kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga
Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka.
Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa changamoto zilizopo
sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo
bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu.
Katiba itakayoimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni
mwa wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na
maeneo watokako, au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama
vya siasa. Katiba itakayodumisha
amani, usalama na utulivu nchini.
Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa
sheria, utawala bora na kudhibiti maovu.
Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka
mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na
maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato
wa kutunga Katiba mpya. Mara ya
kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka
1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato unahusisha
watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na
ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata nafasi ya
kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza
ya Katiba. Pia walipata nafasi ya
kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi
mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba za mwaka
1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama
ilivyo katika mchakato huu. Hata
hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio
waliounda Bunge Maalum. Safari hii
Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi
201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya
Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha
wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977,
mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban
mara 14. Mabadiliko hayo
yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa
na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya
mabadiliko yaliyofanywa:-
1.
Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya
Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka
1977.
2.
Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo
kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
3.
Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo
kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki
za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya
iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya
Muungano.
4.
Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa
ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake
katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika
historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri
Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
5.
Mabadiliko
ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea
Mwenza.
6.
Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo
wa Haki za Binadamu na kuongeza
uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunathibitisha
utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya
hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo
na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya
kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya.
Wako watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno
kiasi kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi
vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai
Katiba mpya kwa imani, eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika
mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika kuwa
baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia
ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada ya
kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala na
Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira
ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na
ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini,
siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika
pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tarehe
16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa
kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza
maoni ya wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na
kupitia Mabaraza ya Katiba.
Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya itakayofikishwa
kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa
wananchi kupiga kura ya maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba
mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012 na
kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa
Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume,
Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe
18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili
kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya.
Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho
kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la
Serikali na magazeti mengine yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika
Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa
wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume
na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo
muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana
na ni kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania.
Pia, kwamba, Watanzania wako huru
kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za
dhati kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino
Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia
ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la
kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya
haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa
Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa
mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika,
walipokea
na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na taasisi
mbalimbali. Baada ya kupokea maoni
ya wananchi, kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya
kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge
hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza
kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao
kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza
Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na
ya manufaa kwa taifa la Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa mapendekezo ambayo kwa
kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya
pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao
na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo,
isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Waheshimiwa
Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa
kilichosheheni mambo mengi. Kina
kurasa 106,
sura 17
na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma
na kuelewa vizuri kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na
umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa
sentensi na hata neno kwa neno.
Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na
kufaa kwa dhana mbalimbali
zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili
kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania
wapate Katiba iliyo bora.
Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu
kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa
na Katiba ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka
ifanyiwe marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee
katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali
zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika hatua
moja kitaonekana katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie
vizuri.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo
mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi
yetu ni kujiridhisha na uandishi wake.
Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba myatafakari na
kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna
baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko
inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo
kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo
yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie
(non justiciable). Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni
mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake
kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe
kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya
Serikali kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine
ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu
sana mambo kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu
kutekeleza.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu
katika uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo
athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya.
Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo
lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania
Bara, sehemu yetu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana
nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa
hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima
mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati
ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu
ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi
washirika. Katika Rasimu hii malengo ya taifa
yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo
yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni.
Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi
na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda,
biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako chini ya mamlaka
ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka
ya Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru
wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu
na kuipa Serikali ya Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha
utata na migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu,
inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili
kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi
washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo
wa Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano
bila ya matatizo. Katika uandishi
wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya
Muungano. Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo
uandishi katika Rasimu. Naamini
mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya
kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi
na mambo mbalimbali. Nawaomba
mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu
kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo
kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza
kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara
ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa
kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita
mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”. Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa
kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na hatia Mahakamani na kuhukumiwa
kifungo. Lakini, isijekuwa yuko
rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo
hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya
kifungo cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa
mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri
mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu
ya “kuugua kwa miezi sita mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili
ambao haustahili kufanywa na Katiba.
Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza kupata ajali
akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake.
Anaweza kuugua kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake
cha Ubunge kufika mwisho. Kwa nini
awekewe ukomo wa miezi sita?
Katiba ya mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa na
sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi?
Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya
yake iimarike ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza
matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni
vyema jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au
hapana.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka
ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge.
Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto
katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha
juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni
kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni
jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika kuungana
na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa
kwetu. Nachelea kuwa tutainyima
nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa
nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya linalopendekezwa na Tume
ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo jema
lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali
wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake
kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao unaweza kuwa
ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni
wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa
thamani inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo hili jipya lina tija. Hivi
kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge
ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu watu
wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya
mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala
mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya
pili. Wakati mwingine mjadala
umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote
katika Rasimu kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa
kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo
agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa
upi. Ombi langu kwenu ni kuwa
watulivu mnapojadili suala hili.
Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili una
hasara kubwa. Tunaweza kupoteza
kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa
migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa
Jaji Joseph Sinde Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa
Serikali tatu si jambo jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha
nchi zetu mbili mwaka 1964.
Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka
1984. Muundo huu uliwahi
kupendekezwa na Tume ya Nyalali
mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji
Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara
zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais
wa Jamhuri ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili tulionao
sasa. Walitoa sababu mbili
kuu: “ni muundo unaoihakikishia
Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo
mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere
asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo
mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika
jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili
na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo
yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe
tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai
yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime
kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na
kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye
uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza
muundo wa Serikali tatu. Sababu ya
kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania
Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya
Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga
mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania
Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika
na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa
na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume
zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo
wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema
Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali
tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi
wape uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi
ukweli huo. Wanasema kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao
kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia
13.6
ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia
86.4 muundo
wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia
13.6
ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe,
kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu
Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu,
asilimia 29.8
walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba
na asilimia 7.7
walipendekeza Serikali moja. Hii hoja
ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile
kuwa Tume ilipokea maoni 772,211.
Kati
ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia
88.6
hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano
ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya
watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia
Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu
Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi
kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa muundo
wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo wa
Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile
kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya
Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania Bara
haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia mkanganyiko
kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano baina ya
Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa
Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Aidha, kuna malalamiko kuwa orodha ya
mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka
mambo 11
mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya
ndani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza
kuwepo kwa manung’uniko kuwa Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho
wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea
maslahi yao ndani ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina
bendera yake, wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar
imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la
Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza
la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki
ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo
Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia
mkanganyiko kuhusu ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za
uendeshaji wa shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya changamoto
ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano
kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba
mfumo wa Serikali tatu utagawanya vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano.
Unawezesha Washirika wa Muungano
kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na hivyo, utawezesha
kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania
kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile
unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia
kukuza maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha changamoto za muundo wa
Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia
kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa na
muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu.
Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza gharama za
uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri
katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi wa pande zetu mbili za
Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo;
na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake
takriban miaka 50 iliyopita (1964).
Aidha, umesaidia kudumisha amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali
Tatu
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Pamoja
na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto za
Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza
kuwa kutakuwa na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa
hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo
tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani
kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (Waulizeni
Wazanzibari) na wala gharama ya
Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya
Shirikisho”.
Ni
matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala
hili kubwa na nyeti.
Tume imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza
kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina
ya nchi washirika. Vilevile, kuna uwezekano
wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya nchi
na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi washirika na
Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti
za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila upande kuwa na
sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya muundo wa
Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika,
hivyo kuweza kudhoofisha Muungano.
Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in
decision making)
katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio
kwa ustawi wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana
ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue Muungano
wenyewe. Changamoto ambazo si
ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali mbili wanasema
kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha
kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali
utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa.
Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza
kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya tatu.
Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia changamoto za
Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za Muungano, Serikali
zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya
Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya
Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye
Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya
Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya
kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1. Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida
ya Benki Kuu.
2. Utafutaji na uchimbaji
mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano wa
Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira kwa watumishi wa
Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5. Usajili wa vyombo vya
moto.
6. Tume ya Pamoja ya
Fedha.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia
fursa ya mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa
kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
1. Utafutaji na uchimbaji
mafuta na gesi asili.
2. Ushirikiano wa
Zanzibar na taasisi za nje.
3. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali kadhalika, katika kipindi cha
mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni nafasi nzuri ya
kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri
ya Muungano. Mimi naishi kwa
matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini
tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazina
kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika.
Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za
Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya
ndani. Na, wala siyo udhaifu wa
viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi yao. La hasha.
Pili, naomba ieleweke kuwa, kila
kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka,
inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye
Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki
za kikatiba na kisheria zilifuatwa.
Hoja ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa
na Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa
Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard
za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli
na undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na
kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya
Mambo ya Muungano. Mambo hayo ni
haya yafuatayo:
1. Katiba ya Jamhuri ya
Muungano,
2. Mambo ya Nje,
3. Ulinzi,
4. Polisi,
5. Hali ya Hatari,
6. Uraia,
7.
Uhamiaji,
8.
Biashara
ya nje na mikopo,
9.
Utumishi
katika Serikali ya Muungano,
10.
Kodi
ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
11. Bandari, Mambo ya
Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano
yaliongezeka kutoka 11 hadi kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali
yaliyotokea nchini na kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano zilikubaliana kuwa mambo hayo
yaongezwe katika Katiba na taratibu za kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe
maelezo kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
1.
Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu,
mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika
tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(East African Currency Board) mwaka 1964.
Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na
sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na
Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee
Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
2. Tarehe 11 Agosti, 1967
yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano:-
(a) Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c)
Jambo
la 15
lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo
ilikuwa na mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la
uratibu. Mambo hayo ni pamoja na
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti,
Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri wa Majini na
kadhalika.
3.
Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali ya
mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na
kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa
jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya
Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
4.
Tarehe
22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani
la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la
Mitihani la Taifa mwaka 1973.
5.
Mwaka
1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya
Mambo ya Muungano ilipangwa upya.
Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano
yalipunguzwa na kubaki matano.
Mambo hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya
Hewa kuwa la 19 na
Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya
Tanzania ikawa jambo la 21.
6.
Tarehe
17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji
wa Vyama vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii
ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa
vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea
nini kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na wala
siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya na
Zanzibar. Kama tulivyoona
mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Kila yalipotokea
mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma
zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba kwa
sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mengineyo yaliachiwa kila upande kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo
yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji
wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ni msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba,
iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya
baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya
hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe
tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo
maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za biashara, utafiti
na mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na imethibitika kuwa
Zanzibar inayamudu. Ni makusudio
yetu kutumia fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi
Asilia
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la
rasilimali ya mafuta na gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu wakati
wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein msimamo
haukubadilika. Kilichotuchelewesha
kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona
kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya
mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza
kukosa majibu.
Hatimaye wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa
umefika. Misemo ya wahenga ya
“subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali
tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa
rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni
binafsi. Pili, kwamba, rasilimali
ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye
mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba,
kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa
Kimataifa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu ambalo Serikali zetu
mbili zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar
kupata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka
nchi za nje bila kizuizi. Kwa sasa
fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi
kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali
ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti
la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache kunufaika
isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar. Serikali
zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa
kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato
huu kuyamaliza mambo haya yaishe!
Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu
mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana,
itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya
au taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka
yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar
bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya
ni kuongeza msukumo, utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza
ipasavyo majukumu yake. Wanaohusika
na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria
au Katiba ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja
inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali
zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana budi upewe nguvu ya
Kikatiba. Tukifanya hivyo
tutafanikiwa kuyaweka mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Waheshimiwa
Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo
wa Muungano wenye Serikali tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri
kuhusu changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya
kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu
wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito
unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali
ya Muungano inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe
za kusimama. Inategemea mno ihsani
ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo
inaweza kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani
ya nchi washirika. Tena inaweza
kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo
cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake.
Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika wa fedha
hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake chenyewe cha
kukusanya mapato hayo. Itategemea
vyombo vya nchi washirika kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama wakati
wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au
kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo
wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana
nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali
ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano
kuvunjika.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano
inapewa fursa ya kukopa kama chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli
zake. Lakini, kwa sababu ya kukosa
rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo kukopesheka. Kwa
jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine
wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa.
Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya
Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais na
Serikali yake watakuwa hawana lo lote la kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni
wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya
Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale
wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na
inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi
yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza
kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na
nchi washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza
kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo.
Kwa waumini wa Serikali
mbili wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika kuainisha changamoto za muundo wa
Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa
ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks
and paralysis)
katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia
za utaifa (nationalistic sentiments) wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana
mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na
uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona hata Tume haikuweza kupata
ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe
mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike kila linalowezekana
kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani yakikwama maana yake shughuli za
Muungano zitakuwa zimekwama. Kama hazitakwamuliwa
kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza
kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia
za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari
ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na kwa
kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi moja yaani Watanzania kwa miaka
50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya Watanganyika na Wazanzibari na
siyo kati ya Watanznaia. Kwa
mujibu wa sensa iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo
sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964.
Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza
kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu
maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa
asili. Wanakuwa wageni na fursa
walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara
moja watajikuta maadui. Aidha, watu
wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa
sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka
huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa mbili za mfumo wa
Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya Tanzania Bara ya
kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za
Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza
kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa
baina ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na
rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana
heri. Umoja wetu utatetereka na
Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa
nini tufike huko?
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya
wananchi wetu, hatuna budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye
uamuzi ulio sahihi. Tusije
tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali zao
kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo
Muungano kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi
kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza
kila kitu tulichokijenga kwa miaka 50.
Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi katika nchi
washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa
kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi
kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle
ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Siku
moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu
ya dini nchini aliniuliza: “Hivi Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza
ya tatu? Si matatizo ndiyo yatazidi?
Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila mtu atachukua njia
yake? Mtakuwa mmepoteza kila
kitu. Mimi nawashauri msichoke
kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni
vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Mambo ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu
ya ufinyu wa muda, nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini,
mtayaona katika kuipitia Rasimu na kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza
kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga Katiba ya nchi ni zito
sana. Taswira ya nchi yetu
itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya kujadili na kuyafanyia
uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana
kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda wa kutafakari kila neno,
kila sentensi, na kila dhana ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi
yetu na Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana kusikia kuwa mtajigawa
kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu
wachache, mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa maoni yao, kwa kila
kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la
kutunga Katiba. Wote mtakuwa
mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki
sifa nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume
chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitamaliza
hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu
Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi,
alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na
ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi
zetu sote. Anastahili pongezi kwa
sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa
Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba kwa hatua mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali
hivyo hamna budi kuongeza kasi. Naomba
niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao
kwenu. Hamna budi, haiba na
taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa lugha na
vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili,
baadhi ya wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo
waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya
baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa
hali ile haitajirudia tena katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na
Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa nchi
yao. Tutoe hoja badala ya kupiga
kelele (argue don’t shout) au kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika
kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili
na lile au hata kugombana. Ni
utovu wa uungwana usiotegemewa
kutoka kwenu. Tusiwaangushe
wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa
wakati wote muongozwe na kujali maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala
ya kujali maslahi yenu binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au
atakuwa nayo kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya
kuleta mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa
tayari kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata
msimamo wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza mawazo ya
wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine
hata kama ni watu usiokubaliana
nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari wa kushawishi badala ya
kulazimisha. Mkifanya hivyo hamtalazimika
kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi maarifa wale
mnaotofautiana nao kwa mawazo.
Lazima pia mtafute namna ya kushirikiana na kuwasiliana na makundi
mengine. Msitafute kushindana,
hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote washinde kwani
wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa
na taratibu za mawasiliano, mashauriano
na ushirikiano. Daima muwe watu wa
kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya
hayo, tafadhalini zitumieni.
Jengeni madaraja imara zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Naomba
nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa dini tumuombe
Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake
waweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila
watakaloliamua.
Baada
ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti
kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni kila la heri na mafanikio
mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu
Wako.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge Maalumu la
Katiba!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!

No comments:
Post a Comment