MTOTO WA KIKWETE AANZA KAMPENI KUWANIA UBUNGE CHALINZE...

Ridhiwani Kikwete katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
Wakati leo ni siku ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, mgombea wa ubunge katika uchaguzi mwingine mdogo jimboni Chalinze, Pwani kwa tiketi ya CCM, Ridhiwani Kikwete jana alianza kwa kishindo kampeni zake.
Katika kampeni hizo, alifanikiwa kuivunja ngome ya Chadema katika kijiji cha Saadani baada ya mwenyekiti wake na wajumbe wawili kuhamia CCM, wakidai vyama vya upinzani haviaminiki.
Miongoni mwa ahadi zake alizozitoa katika kijiji cha Matipwili katika siku ya kwanza ya kampeni ni kuhakikisha wakazi wa kijiji hicho watakaopisha ujenzi wa barabara ya Afrika Mashariki wanalipwa kwa wakati fedha zao.
Aidha, ameahidi kuzikabili changamoto mbalimbali za wananchi wa jimbo hilo endapo watamchagua kwenye nafasi hiyo.
"Nawaomba mnipe ridhaa yenu ya kuongoza kwa kunichagua ili niweze kuwasaidia katika changamoto hii na nyingine ambazo zinawakabili lakini la kwanza ni hili la malipo ya nyumba zenu ambazo zitabomolewa kupisha ujenzi wa barabara ya Afrika Mashariki," alisema.
Aliongeza kuwa, atazikabili changamoto kwa kuwa kazi ya Mbunge ni kufuatilia matatizo ya wananchi na kuangalia namna ya kuweza kupata wahusika wa kuzitatua ikiwa ni pamoja na halmashauri na wahisani mbalimbali wa maendeleo.
"CCM ndiyo yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo na msikubali kuchagua wapinzani kwani hawana uwezo wa kuwasaidia zaidi ya kuwarubuni na kuwalaghai tu hawataweza kuleta maendeleo," alisema.
Aidha alisema kuwa changamoto zilizopo kwenye sekta za elimu, afya, maji, miundombinu na kilimo ni vipaumbele vyake ambavyo atahakikisha anazifanyia kazi endapo watamchagua kwenye nafasi hiyo.
Kwa upande wa Meneja wa Kampeni wa jimbo hilo, Steven Kazidi alisema kuwa CCM ndicho chama kinachoongoza Serikali hivyo wananchi wanapaswa wasifanye makosa kuwachagua wapinzani ambao hawana uwezo wa kuongoza.
Licha ya kuanzia kampeni zake Matipwili, Kikwete alifanya pia kampeni katika vijiji vya Gongo, Mkange na Saadani. Akiwa katika kijiji cha Saadani, Mwenyekiti wa Chadema wa kijiji hicho, Bakari Mfaume na wajumbe wake, Gema Aloyce na Abdallah Ismail walitangaza rasmi kuhamia CCM. Uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM utafanyika Chalinze Jumamosi ijayo.

No comments: