JAMBAZI AFIA KWA MGANGA WA KIENYEJI TARIME...

Mkazi wa Kijiji cha Kemakorere, Kata ya Nyarero iliyopo Tarafa ya Inchage, Tarime, Nchagwa Marwa Yusuph (35) aliyekuwa akisakwa kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha wilayani hapa, amekutwa amekufa nyumbani kwa mganga wa kienyeji alikokuwa akitibiwa majeraha.
Hata hivyo, mganga huyo anayefahamika kwa jina la Marwa Wambura alifanikiwa kuwatoroka polisi waliovamia nyumba yake baada ya kuelezwa juu ya uwepo wa jambazi huyo.
Tukio hilo limethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Sweetbert Njewike.
Akizungumza ofisini kwake, alisema: "Tulipata taarifa kutoka kwa raia wema  Ijumaa ya Machi 14 mwaka huu juu ya  kuonekana kwa mtuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha na wizi wa mifugo, Nchangwa Marwa Yusuph akiwa anatibiwa kwa mganga wa kienyeji Marwa Wambura katika kijiji cha Kemakorere.
“Waliomwona mtuhumiwa wanasema alikuwa anatibiwa majeraha ya kukatwa mapanga kichwani na sehemu mbalimbali za mwili. Na kweli, tulikwenda na kumkuta akiwa hoi kutokana na kuvuja damu nyingi, licha ya kuwa alifungwa kitambaa kichwani na kuwekewa dawa za mitishamba. Alifariki muda mfupi baadaye wakati tukiwa katika harakati za kumpeleka hospitali ya wilaya.”
Kamanda huyo aliongeza kuwa, walipofika kwa mganga huyo hawakumkuta, kwani aliwatoroka na kwamba msako mkali dhidi yake unaendelea ili akamatwe na kuburuzwa kortini kwa tuhuma za kuhifadhi wahalifu.

No comments: