Monday, March 3, 2014

MGOGORO WA UONGOZI CHADEMA SASA WAGEUKA KITUKO...

Mbunge Said Arfi.
Mgogoro wa uongozi ndani ya Chadema, umeingia  katika  hatua  nyingine baada ya makada wa chama hicho   wanaopingana kimisimamo, kufunga ofisi  za chama hicho  mjini Mpanda kwa zaidi ya wiki sasa.

Makada  hao  wamegawanyika na kuwa  na kambi  mbili  tofauti, ambapo  kila  upande umeweka  kufulia  lake na   walinzi wake, kuhakikisha  hakuna  atakayevunja na kuingia  ofisini humo.
Ofisi  za chama hicho  ambazo  ziko katika Mtaa wa Mji wa  Zamani  mjini hapa,  kabla ya kufungwa zilikuwa  zikitumiwa  na viongozi  wa chama hicho  ngazi ya wilaya  na mkoa pamoja na  viongozi  Jimbo la Mpanda Mjini, ambalo kwa  sasa Mbunge  wake  ni Said Arfi (Chadema).
Mvutano  huu wa uongozi, uliibuka mwanzoni mwa  wiki iliyopita,  ambapo viongozi  wa chama hicho  waliosimamishwa  hivi karibuni, walifika ofisini  hapo   ili waendelee na  shughuli zao  za kiofisi  na kukuta ofisi zimefungwa  kwa  kufuli  lingine  tofauti na waliloliweka wao.
Baada ya kubaini  hivyo,  viongozi hao  wa Jimbo la Mpanda Mjini,  walilazimika kuwahoji  wenzao wa wilaya  kulikoni  ofisi  za chama hicho kufungwa  kwa kufuli  lingine, tofauti na hilo, ndipo walipojibiwa  kuwa  wao si viongozi tena, kwa kuwa tayari wamesimamishwa  uongozi.
Pia,  uongozi  wa wilaya wa chama hicho,  wanadaiwa kuwajibu  wenzao  hao kuwa kwa kuwa wamesimamishwa uongozi,  hawana  mamlaka tena  ya  kufanya shughuli  zozote  za  chama  ndani  ya ofisi hizo.
Hivi karibuni kikao cha maridhiano ya chama hicho,   kilichofanyika  kwenye ofisi cha  chama  hicho  zilizopo  katika mtaa wa Mji wa Zamani  mjini hapa, kiliwasimamisha  uongozi  baadhi ya  viongozi  waandamizi  wa chama hicho mkoani hapa  na wengine wawili  kusimamishwa uanachama.
Kikao hicho kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti  wa Chadema Kanda Magharibi , Masanja Katabi, kiliwasimamisha uongozi Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Katavi, John Malack, Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoani hapa , John Matongo na Mwenyekiti wa Jimbo la Mpanda Mjini, Seif Sipia.
Wengine ni Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini Joseph Mona, ambaye pia ndiye Katibu wa Mbunge, Arfi na Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini, Godfrey Kapufi.
Mbali ya kusimamishwa uongozi, kikao hicho kimependekeza Kapufi na Diwani wa Kata ya Makanyagio, Idd Nziguye wavuliwe uachama,  kama ilivyokuwa kwa akina Dk Mkumbo na Mwigamba.
Pia, kikao hicho pia kiliazimia Arfi achunguzwe, wakimtuhumu kudhamini mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Maridadi mjini hapa,
unaodaiwa kutumika kuwakashifu Lema na Mnyika.

No comments: