Wednesday, March 12, 2014

MCHUNGAJI MTIKILA, MKOSAMALI WACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI...

Felix Mkosamali (kushoto) na Mchungaji Christopher Mtikila.
Mwenyekiti wa chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) 'wamechafua hali ya hewa bungeni' wakilalamikia kutopewa nafasi ya kuchangia azimio la kupitisha rasimu ya kanuni ya kuliongoza bunge hilo Maalum la Katiba.

Aliyeanza kutoa malalamiko yake na kusababisha wajumbe wa bunge hilo baadaye kumzomea ni Mtikila ambapo baada ya Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho kumaliza kuwapa nafasi wachangiaji, alisimama na kusema, "Kwa nini huniruhusu na mimi kuzungumza, kwa nini unanizuia kuzungumza".
"Unataka nikuheshimu wakati heshima yangu unaivunja. Ni haki yangu kuzungumza nahitaji jibu uniambie kwa nini hunipi nafasi kuzungumza. Unachagua mtu azungumze unachofurahia wewe hapa ndani, hujui maneno yangu yanaweza kulinusuru taifa, na mimi nipe nafasi nizungumze sikuombi ni haki yangu Neno haki limenenwa mara nyingi humu ndani ya bunge na ni katika misahafu imesemwa haki ni ufalme wa Mungu, wewe humuamini Mungu," alisema.
Baada ya kumaliza kukasikika sauti ikisema, "huna nidhamu Mtikila".
Alipomaliza bila kuruhusiwa akasimama Mkosamali na kusema, "na mimi pia umeninyima nafasi ya kuzungumza, unawapa nafasi mnaokubaliana cha kuzungumza si haki katika kutengeneza katiba, mnapitisha kanuni mbovu".
Na yeye baada ya kumaliza kuzungumza ikasikika sauti ikisema, "kaa chini huna nidhamu".
Kutokana na kauli za wajumbe hao zilizosababisha zomea zomea ndani ya bunge, Kificho akasema kuwa wajumbe ni wengi walioomba nafasi ya kuzungumza katika kupitisha azimio hilo la kupitisha kanuni na yeye akachagua wachache na kuomba radhi kwa waliokosa nafasi hiyo.
Waliopewa nafasi ya kuzungumza wote waliunga mkono hoja ya kupitishwa kwa kanuni hizo pamoja na kanuni ya 37 na 38 zinazoeleza maamuzi yote yatapitishwa kwa kupigiwa kura bila kutaja aina ya kura kama ya wazi au ya siri na uamuzi huo utapatiwa ufumbuzi wakati wowote wakati shughuli ya kujadiliwa kwa rasimu ya katiba ikiendelea.
Wajumbe hao waliozungumza ni Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kutoka makundi mbalimbali, Dk Francis Michael, Jenister Mhagama, Idrisa Kitwana Mustafa, James Mbatia, Panya Ali Abdalla, Frederic Msigalla, Vuai Ali Vuai, Shehe Mussa Kundecha, Freeman Mbowe, Ismail Jussa, Askofu Amos Mhagachi na mtoa hoja ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya kanuni, Profesa Costa Mahalu.
Hata hivyo, wakati wa kupitishwa kwa kanuni hizo licha ya wajumbe wengi kusimama kuunga mkono, Mtikila na Mkosamali hawakusimama.

No comments: