Sunday, March 2, 2014

KARDINALI PENGO ATOA ONYO KALI BUNGE MAALUM LA KATIBA...

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa mara ya kwanza amezungumzia Bunge Maalum la Katiba na kuwaonya Wajumbe wa Bunge hilo kutowagawa Watanzania wakati wa mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.

Sambamba na hilo, amewataka wajumbe hao na viongozi wa Serikali kwa ujumla kutoiweka amani ya nchi hatarini bali kutambua kuwa Watanzania wanataka Katiba itakayowawezesha kuendelea kuwa wamoja.
Aidha, amesema ingawa hali ya amani kwa sasa inaridhisha, lakini matukio ya uvunjifu wa amani bado yanatokea na kuwakumbusha Watanzania kuwa hitaji la pekee kwa sasa ni kuzingatia misingi ya umoja na amani iliyojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Kardinali Pengo aliyasema hayo jana, Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya Ibada ya Misa ya kutabaruku altare na kubariki jengo la Kanisa la Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, Magomeni lililokarabatiwa kwa miaka mitatu.
Pengo alisema, "Wosia wangu kwa wajumbe ni kumuomba Mungu shughuli nzima ya kupata Katiba aifanikishe mwenyewe, tunahitaji Katiba ya kutulinda katika umoja."
"Viongozi wa sasa na wajao wakumbuke hili kwamba Watanzania tunapenda kubaki wamoja, si vipande vipande, bali wamoja, wasiweke maslahi binafsi mbele bali ya Taifa ndio yawe mbele," alisema Pengo.
Ingawa hakutaja maeneo anayoona yanaelekea kuvunja amani ya nchi ama kuondoa umoja uliopo, lakini kwa wiki mbili sasa, wajumbe wa Bunge Maalum wamekuwa wakijadili Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo huku suala kubwa likiwa ni namna ya upigaji kura, wengine wakitaka uwe wa siri huku wengine wakitaka uwe wa wazi.
Pia suala la posho lilichukua nafasi kubwa katika wiki ya kwanza ya vikao vya Bunge hilo huku baadhi ya wajumbe wakidai Sh 300,000 wanayolipwa haitoshi. Jambo jingine ni muundo wa serikali ya Muungano ama uwe wa serikali tatu, mbili au moja, ambao mpaka sasa unadaiwa kuwa jambo litakalochukua nafasi kubwa katika Bunge hilo la Katiba.
Akizungumzia amani, Pengo alisema, "Amani inarejea lakini nimesikia kwenye Redio Tumaini asubuhi (jana) kuwa Shehe Mkuu wa Msikiti mjini Arusha kamwagiwa tindikali, hii bado ni hali mbaya, nadhani Watanzania tunapaswa kusikiliza aliyosema Robert Mugabe (Rais wa Zimbabwe) kwamba sisi tulirithi kitu kikubwa sana kwa Nyerere".
Pengo alisema akimnukuu Mugabe kuwa, moja ya mambo Watanzania waliyorithi ni umoja na amani hivyo ni hatari kuiweka amani ya nchi hatarini na kuacha watu wa nje waonekane wanamstahi zaidi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuliko Watanzania wenyewe, ni fedheha.
Mapema mwaka huu, Mugabe katika moja ya hotuba yake nchini mwake, alimwelezea Mwalimu Nyerere kama shujaa wa Afrika aliyehusika katika ukombozi wa nchi nyingi ambaye Mataifa ya Afrika hayajatambua thamani yake na kutaka aenziwe na kuheshimiwa.
Awali akihubiri katika Ibada ya Misa, Pengo aliwapongeza waumini wa Parokia hiyo kwa kujitolea, fedha na mali zao kujenga kanisa na kuwataka liwe kweli eneo takatifu na kimbilio la watu kutafuta amani, kusamehewa, kupona na utakatifu huku akiwataka kutochoka kujenga makanisa kwa kuwa ni kutimiza agizo la Mungu.
Alipotabaruku altare, alizika madhabahuni hapo masalia ya mabaki ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda na kisha kufukiza ubani ikiwa ni ishara ya kupeleka shukrani kwa Mungu na kuweka wakfu usimamizi wa kanisa hilo kwa mashahidi hao na Yesu Kristo mwenyewe.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Matumaini alisema ukarabati huo umegharimu Sh bilioni 1.25 ambazo waumini walijitolea kwa fedha, mali na sala. Alisema ukarabati ulifanyika kwa miaka mitatu na sasa kanisa linaweza kuingiza watu kuanzia  1,500 hadi 2,000 kutoka 1,000 wa awali.

No comments: