Wednesday, March 5, 2014

JANE MAGIGITA ATUNUKIWA TUZO LA MARTIN LUTHER KING...

Jane Magigita.
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya Equality for Growth (EfG), Jane Magigita, ametunukiwa na Ubalozi wa Marekani nchini tuzo ya Haki ya Dk Martin Luther King kwa mwaka 2014, kwa kutambua jitihada zake katika kutetea haki za kisheria za wanawake.

Katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Magigita alitunukiwa tuzo hiyo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser.
Tuzo hiyo imetokana na jitihada zake  za kutetea wanawake, hususani katika kukabili tatizo la ukatili wa kijinsia, urithi na matumizi ya ardhi kwa wanawake vijijini.
Blaser alisema Magigita amepatiwa tuzo hiyo baada ya jitihada zake za kuonekana,  ambapo kwa miaka 13 amekuwa akitoa huduma ya msaada wa kisheria kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Kama ilivyo kwa Dk King alitumia muda wake na nguvu zake katika kuhamasisha amani na usawa na kutetea haki za wanyonge, hivyo na sisi tunazitambua jitihada hizi za Magigita kwani wanawake hawa na watoto wao wameweza kukataa uonevu unaoambatana na ukatili wa kijinsia,” alisema Blaser.
Alisema kama ilivyo kwa Dk King, Magigita katika utekelezaji wa malengo yake ya kutetea haki za wanawake, haogopi kutumia mivutano iliyopo katika jamii kama fursa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii husika.
Alisema  katikati ya mila, tamaduni na imani zinazomkandamiza na kumyima haki mwanamke zilizoota mizizi katika jamii kwa muda mrefu, bado Magigita mwaka 1999 aliweza kufanyakazi na kushawishi wazee na viongozi wa kimila vijijini, viongozi wa wilaya na mikoa na kuwezesha kupitishwa kwa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 inayosaidia kulinda haki ya wanawake Tanzania.
Kwa upande wake,  Magigita alishukuru kwa kutunukiwa tuzo hiyo. Alisema tuzo hiyo imempatia hamasa na kutambua kuwa kazi zake zinaonekana na kukubalika, lakini pia zimefanikiwa kuleta mabadiliko katika jamii.
Alisema anapokea tuzo hiyo kwa niaba ya wanawake wote wa Tanzania, wanaofanyakazi katika sekta isiyo rasmi na kufanya shughuli zao katika mazingira magumu huku wakitoa mchango mkubwa katika jamii, lakini bado wakiendelea kunyanyaswa na kuwekwa pembeni.
Watu wengine waliowahi kutunukiwa Tuzo ya hiyo ya Haki ya Dk Martin Luther King Jr. ni pamoja na Joseph Warioba mwaka 1999, Mwalimu Julius Nyerere (baada ya kufariki) mwaka 2000, Francis Nyalali mwaka 2002,  Profesa Geoffrey Mmari mwaka 2003,  Justa Mwaituka mwaka 2004, na Balozi Gertrude Mongela mwaka 2005.
Wengine ni Dk Salim Ahmed Salim (2006),  Rashid  Kawawa (2007),  Reginald Mengi (2008),  Jumuiya ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) Tanzania (2009), Dk Marina Njelekela (2010), Kamati ya Watu Sita ya Zanzibar iliyowezesha kura za maoni kuhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (2011) na Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani  mwaka jana.

No comments: