BEI YA GESI KUSHUKA KWA ASILIMIA 50...

Mitungi ya gesi.
Bei ya gesi ya kupikia inatarajia kupungua bei kwa nusu baada ya Serikali kutarajia kujenga mtambo wa kusindika gesi hiyo.
Aidha, Shirika la Umeme la Algeria linatarajia kuanza kusambaza umeme nchini kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alibainisha hayo jana baada ya kikao chake na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria ,Youcef Yousfi na wataalamu wa wizara hizo mbili.
Alisema hatua hizo ni kati ya miradi mingi ya ushirikiano katika sekta hizo, ambapo ujenzi wao ukikamilika utapunguza gharama kwa asilimia 45 au nusu ya gharama ya sasa.
Profesa Muhongo alisema Algeria ina uzoefu katika kusindika gesi asilia ambapo kwa mwaka jana pekee ilisambaza gesi hiyo tani  milioni 115 mijini na vijijini nchini humo.
Alisema wamekubaliana na wataalamu kuwa ifikapo Juni 30 kwenye mkutano wa kuandaa miradi hiyo utakaofanyika Algeria, wataalamu wapeleke namna ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Wataalamu watueleze  eneo wanalopendekeza kujenga kiwanda, gharama za ujenzi, masoko ya gesi pamoja na teknolojia itakayotumika ili kufahamu gharama za uwekezaji huo,” alisema Muhongo.
Alisema kutokana na kiwanda hicho, Watanzania wataachana na matumizi ya mkaa na kuni, jambo litakalosaidia uhifadhi wa mazingira.
Alisema kampuni za nchi hizo zinazohusika na masuala ya gesi zitahusika katika kujengwa kwa mitambo hiyo na uendeshaji wao.
Akizungumzia usambazaji umeme alisema kampuni hizo mbili zitashirikiana kusambaza umeme mijini na vijijini na kisha kushirikiana katika ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme masafa marefu.
Profesa Muhongo alisema pia Algeria ina utaalamu na uzoefu mkubwa katika madini, na hivyo itaanzisha migodi ya Fosiforasi kutengeneza mbolea na kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Alisema nchini kuna aina nyingi ya madini hayo, lakini hakuna utaalamu wa kuyatumia ambapo kwa sasa inatengenezwa mbolea ya aina moja ya Minjingu.
Alisema pia nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika utunzaji wa takwimu na taarifa.
Waziri Muhongo alisema ili kusaidia Watanzania kuwa na wataalamu wake, Algeria inatoa ufadhili wa mafuta na gesi kwa vijana na kwa kuanzia, mwaka jana walikwenda vijana 50,  mwaka huu 60.
Waziri Yousfi alisema ushirikiano huo wa kiuchumi hautaishia katika miradi hiyo pekee bali itakuwa na wigo mpana zaidi.
Alisema katika nchi yake yenye wananchi milioni 38 asilimia 98 wanapata   umeme majumbani huku idadi kubwa ikitumia gesi kupikia.
Alisema nchi yake imevutiwa kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kutokana na ushirikiano wa kisiasa uliopo kwa miaka mingi baina ya nchi hizo mbili, kuwapo rasilimali nyingi na utulivu wa kisiasa.
Alisema nchi yake inatarajia kufaidika na uzoefu wa masuala ya madini ambayo Tanzania inayo huku zikibadilishana uzoefu katika masuala   ya kiuchumi.

No comments: