WABUNGE WAMKOMALIA MWANDISHI WA UINGEREZA AOMBE RADHI...

Wabunge nchini wamesema habari ya Gazeti la Uingereza la Daily Mail on Sunday kuwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inafumbia macho ujangili ni upotoshaji na serikali inapaswa kumtaka mwandishi huyo aombe radhi.
Pia wamesema habari hiyo kutolewa haraka bila kuulizwa upande wa pili –serikali ya Tanzania - huku kukiwa na kikao kuhusu masuala hayo nchini humo ni mwendelezo wa vyombo vya Magharibi kutozitakia heri nchi  changa.
Umoja wa Wabunge Unaoshughulikia  Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira nchini, ulieleza hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari kuwa gazeti hilo halijui kinachotokea nchini dhidi ya ujangili wa tembo na faru.
Katibu wa Umoja huo, Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba alisema kutokana na habari hiyo mkutano wa leo unaohusu uhifadhi wa viumbe hai unaofanyika Uingereza unamvua nguo Rais, kwani habari ile ilidai kuwa kuwa mikono yake inanuka damu ya tembo na faru kwa nia ya kupata fedha za uchaguzi wa mwakani.
“Jambo la kujiuliza ni kwa nini habari hii itoke haraka kiasi hiki kabla ya mkutano wa kesho (leo), huu ni udhalilishaji na tunaiomba Serikali imtake mwandishi aombe radhi kwani alichoandika si cha kweli na pengine ana ajenda ya siri,” alisema Mabumba.
Pia alizungumzia suala la Waziri Kivuli wa Maliasili, Peter Msigwa (Chadema) kukaririwa na gazeti hilo akisema Serikali haifanyi kitu katika kukabiliana na ujangili. Mabumba alisema kitendo cha mbunge huyo kinadhihirisha asivyo Mzalendo kwa nchi yake.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo wenye wajumbe zaidi ya 20, Mbunge wa Igalula,  Athuman  Mfutakamba, alisema watajadiliana na Bunge ili kutoa azimio la pamoja kuhusu habari hiyo.
Alisema ni ukweli kuwa biashara hii  haramu ya ujangili wa tembo na faru inafanywa na mataifa makubwa, huku Rais akiwa mstari wa mbele kuipinga hata akaidhinisha Operesheni Tokomeza Ujangili.
“Umoja wetu umeshtushwa na taarifa za gazeti hili, kwani Rais aliagiza faru kutoka nje ili waendelee kuvutia watalii na kuchangia pato la Taifa ambalo kwa mwaka huiingizia Tanzania fedha nyingi za kigeni,” alisema.
Mfutakamba alisema kutokana na juhudi za Rais Kikwete kutumia vyombo vya usalama, mwaka jana kuna kesi 322 mahakamani huku zikikamatwa tani 12 za meno ya tembo.
Katika Daily Mail on Sunday la Februari 8-9 mwandishi Martin Fretcher alihoji kama itakuwa halali kwa Mwana Mfalme Prince William na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kupeana mikono na Rais Kikwete kwenye mkutano huo wa kimataifa unaoanza leo, Lancaster House jijini London.
Mwandishi huyo alionesha kutoridhishwa na Rais Kikwete kupewa mapokezi makubwa katika kikao hicho cha kudhibiti ujangili kwa kuweka mikakati ya kuwinda wanyamapori hasa tembo na faru wasiangamie kutokana na vitendo vya ujangili.
Katika mwendelezo wa kupotosha, alidai kwamba Kikwete hana juhudi wala mikakati ya kulinda wanyama hao.

No comments: