SIKU MBILI KABLA, CHADEMA YATISHIA KUSUSIA BUNGE LA KATIBA...

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akifurahia jambo na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.
Wakati keshokutwa Bunge  Maalum la Katiba linaanza kukutana mjini Dodoma, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema huenda kikasusia Bunge Maalum la Katiba iwapo litaendeshwa kwa kufuata matakwa ya chama cha siasa na siyo ya wananchi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema hayo jana wakati akielezea maamuzi ya Kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika jana na kueleza kuwa chama hicho kinaenda katika Bunge hilo kikiwa na hadhari ya hilo.
Alisema wanaenda kwenye kikao hicho wakiwa na masikitiko kutokana na uteuzi wa wajumbe 201 wa bunge hilo waliotangazwa hivi karibuni kuwa karibu asilimia 75 hadi 80 ni wanaCCM.
Akijibu hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema “Tumewazoea, sio mara ya kwanza kususa waache wasuse najua nia yao tangu mwanzo ni Katiba isipatikane. Katiba mpya itapatikana hata wakisusa”.
Naye Mbowe alifafanua “Hatuendi katika bunge hilo kugoma lakini mambo yakienda visivyo kwa kufuata matakwa ya chama cha siasa na siyo mapendekezo ya rasimu ya pili ya Katiba hiyo ambayo ni ya wananchi tutalizira Bunge hilo,” alisema.
Alibainisha kuwa chama hicho hawatasita kurejea kwa wananchi wakati Bunge likiendelea au likiwa limeisha iwapo wingi wa wabunge wa chama tawala utaathiri Bunge hilo.
“Sasa wananchi watatuelewa dhamira yetu ya kutaka wajumbe hao wasiteuliwe na Rais kwani tulibishana sana lakini baadaye tulikubaliana jambo ambalo limeonesha kwa kuteuliwa makada wengi kwa manufaa ya chama tawala,” alisema Mbowe.
Alisema ingefaa makundi yenyewe yangeteua wawakilishi wao na siyo kupeleka kwa Rais hivyo Bunge hilo linaloanza keshokutwa wanaenda kwa tahadhari.
Vikao vya Bunge Maalum la Katiba linatarajia kuanza keshokutwa likihusisha wajumbe ambao ni wabunge wote wa Baraza la Wawakilishi ,Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete akishirikiana na Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein.
Wajumbe hao 201 wameteuliwa kutoka makundi tofauti yakiwemo ya Taasisi zisizo za kiserikali, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Taasisi za dini, Taasisi za elimu, watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wakulima, wafugaji, wavuvi na kundi la watu wenye malengo yanayofanana.
Bunge hilo litahusisha wajumbe takriban 650 wanaokwenda kuijadili rasimu ya pili ya Katiba na watatumia siku 70 na iwapo hazitatosha wataongezewa siku 20 ili kukamilisha mjadala huo.
Kitakachofuata baada ya Bunge Maalum la Katiba ni wananchi kupiga kura ya maoni kupitisha Katiba hiyo mpya. Katiba hiyo mpya itafuta Katiba ya sasa iliyodumu tangu Tanganyika  ilipopata uhuru mwaka 1961 na mabadiliko kadhaa yaliyofuatia baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema “tumewazoea, sio mara ya kwanza kususa waache wasuse najua nia yao tangu mwanzo ni Katiba isipatikane. Katiba mpya itapatikana hata wakisusa”.

No comments: