Ndege hiyo mara baada ya kutua. |
Ndege hiyo aina ya Boeing 767-300 ikiwa na abiria 202 na wafanyakazi ndani yake iliruka kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, na kutua kwenye mji huo wa Uswisi majira ya saa 12 asubuhi. Maofisa walisema hakuna yeyote ndani ya ndege hiyo aliyejeruhiwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uwanja wa Ndege wa Geneva, Robert Deillon aliwaeleza waandishi wa habari kwamba rubani huyo msaidizi, raia wa Ethiopia aliyezaliwa mwaka 1983, aliidhibiti ndege hiyo pale rubani alipotoka nje ya chumba cha marubani.
"Rubani huyo alikwenda msalani na (rubani huyo msaidizi) akajifungia ndani ya chumba cha marubani," alisema Deillon.
Mtu huyo "aliomba hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa nchini Uswisi," alisema. "Hicho ndicho kichocheo cha utekaji nyara huo."
Utekaji nyara huo ulianzia Italia, jirani wa Uswisi kwa upande wa kusini, na ndege mbili za kivita za Italia ziliambatana kuisindikiza ndege hiyo, kwa mujibu wa Deillon.
Maofisa wa polisi walimsaidia abiria mmoja kutopanda ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia iliyotekwa yenye usajili wa ET 702 kwenye Uwanja wa ndege wa Cointrin.
Abiria kwenye ndege hiyo hawakufahamu lolote kwamba ndege hiyo ilikuwa imetekwa, maofisa walisema.
Dakika chache baada ya kutua mjini Geneva, rubani huyo msaidizi alitoka kwenye chumba cha marubani kwa kutumia kamba, "kisha akajipeleka kwenye vikosi vya polisi ambao walikuwa chini karibu kabisa na ndege hiyo," msemaji wa polisi wa Geneva Eric Grandjean alisema. "Alitangaza kwamba yeye mwenyewe ndiye alikuwa mtekaji."
Haikuweza kufahamika mara moja kwanini rubani huyo msaidizi, ambaye jina lake halikuwekwa hadharani, alikuwa akitaka hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa.
Polisi waliwasindikiza abiria mmoja baada ya mwingine, mikono yao ikiwa kichwani, kutoka kwenye ndege hiyo kuelekea kwenye magari yaliyokuwa yakiwasubiria.
Mwendesha mashitaka wa Geneva Olivier Jornot alisema mamlaka za Uswisi zilikuwa zikichunguza utekaji huo na utafungua mashitaka ambayo yanaweza kupelekea hukumu ya kifungo cha hadi miaka 20 jela.
Uwanja wa Ndege wa Geneva ulifungwa kwa muda kwa ndege nyingine, lakini shughuli ziliendelea takribani masaa mawili baada ya ndege hiyo iliyotekwa nyara kutua.
Shirika la Ndege la Ethiopia linamilikiwa na Serikali ya Ethiopia, ambayo imekuwa ikikumbana na shutuma za mara kwa mara kuhusiana na kumbukumbu za haki zake na madai ya kukosa uvumilivu wa tofauti za kisiasa.
Kumekuwa na utekaji nyara mwingi unaofanywa na Waethiopia, wengi wanaotoroka kwa wingi kwenda mataifa ya Afrika Mashariki ama kuhofia kurejea makwao.
Raia mmoja wa Ethiopia alisafiri na bastola ndani ya ndege ya Lufthansa na kuiteka nyara ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Frankfurt kwenda Addis Ababa mwaka 1993. Alitaka ndege hiyo badala yake ielekee Marekani sababu alikuwa amenyimwa viza.
Mnamo Juni na Aprili mwaka 1994, Shirika la Ndege la Ethiopia lilikabiliwa na matukio ya utekaji nyara miongoni mwa abiria ambao walitaka kupelekwa Ulaya. kwa mujibu wa Mtandao wa Usalama wa Anga, ambao unafuatilia utekaji nyara na matukio mengine.
Mwaka 1995, raia wa Ethiopia akijaribu kuepuka kurejeshwa kwao alitumia kisu alichochukua kwenye kasha la chakula kuishurutisha ndege ya Shirika la Ndege la Olympic muda mfupi kabla haijatua mjini Athens, Ugiriki. Polisi walimzidi nguvu mtekaji huyo bila kujeruhi yeyote kati ya abiria 114 waliokuwamo ndani, kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la AP.
Pia mwaka huohuo, watu watano wenye silaha waliiteka ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kuitaka ndege hiyo kuruka kwenda Ugiriki na kisha Sweden. Badala yake ilibadili mwelekeo na kwenda Al Obeid, takribani maili 300 (kilometa 480) magharibi mwa Khartoum, Sudan.
Mwaka 1996, ndege moja iliyokuwa ikitokea Ethiopia kwenda Ivory Coast kupitia Kenya ilinaswa na watekaji nyara ambao walitaka iende Australia. Ndege hiyo iliishiwa mafuta na kuanguka kwenye kisiwa cha Comoro, na kuua watu 125, kwa mujibu wa Mtandao wa Usalama wa Anga.
Mwaka 2001, marubani watano wa kijeshi waliokuwa mafunzoni ambao walirusha ndege waliripotiwa kushindwa kuidhibiti ndege hiyo wakati wakiruka kutoka Bahr Dar, kaskazini-magharibi mwa Ethiopia, kwenda mji mkuu wa Addis Ababa na kutaka wapelekwe Saudi Arabia. Ndege hiyo haikuwa na mafuta ya kutosha hivyo ikalazimika kutua katika nchi ya jirani ya Sudan, kwa mujinu wa ripoti za AP.
Mwaka 2002, abiria wawili waliobeba visu vidogo na mabomu walijaribu kuteka ndege ifanyayo safari za ndani lakini walipigwa risasi na kuuawa na mlinzi wa ndani ya ndege, Mtandao wa Usalama wa Anga uliripoti.
No comments:
Post a Comment