EWURA YAPATA MKURUGENZI MKUU MPYA...

Felix Ngamlagosi.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imepata Mkurugenzi Mkuu mpya, Felix Ngamlagosi.

Taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Ewura, Simon F. Sayore, ilieleza kuwa uteuzi huo umefanywa na Waziri wa Maji, Profesa  Jumanne Maghembe na ulianza rasmi Februari mosi mwaka huu.
Ngamlagosi anachukua nafasi iliyoachwa na Haruna Masebu, aliyemaliza muda wake Desemba 31 mwaka jana, baada ya kuitumikia Mamlaka kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja, kwa mujibu wa Sheria ya Ewura.  
Kabla ya uteuzi wake,  Ngamlagosi alikuwa Mkurugenzi wa Udhibiti wa Kiuchumi wa Ewura, nafasi aliyoitumikia kwa miaka saba.
Ngamlagosi ana Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uchumi, kutoka Moscow Finance Academy, aliyoipata kati ya 1990  na 1996 nchini Urusi na Stashahada ya Uandaaji Sera na Miradi ya Maendeleo mwaka 2000 kutoka Taasisi ya Elimu ya Jamii (ISS), The Hague  nchini Uholanzi.
Pia Ngamlagosi alipata elimu ya Fundi Mchundo kutoka Chuo cha Maji (1984 Ð 1987) na ana Tuzo ya Uzamili Bingwa kwenye Udhibiti wa Huduma za Kiuchumi, iliyotolewa kwa pamoja kati ya  Taasisi ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi ya Washington, Marekani na Kituo cha Maji, Uhandisi na Maendeleo cha Chuo Kikuu cha Loughborough (WEDC/LU) cha Uingereza (2013).
Mbali na elimu hiyo, Ngamlagosi ana utaalamu wa masuala ya udhibiti wa huduma za nishati na maji, akiwa amebobea kwenye uchambuzi wa bei za huduma, ufuatiliaji wa taasisi zinazotoa huduma, mbinu za kulinda maslahi ya watumiaji na uandaaji wa mifumo ya mawasiliano na wadau katika sekta za umeme, petroli, gesi asili na maji.
Kabla ya kujiunga na Ewura,  Ngamlagosi alifanya kazi Wizara ya Maji, Nishati na Madini na baadaye Wizara ya Maji kwa miaka 17, akipanda vyeo mbalimbali hadi kuwa Mchumi Mwandamizi.
Pia, alichangia kazi za kitafiti, kama mtaalamu-mwenza, za Uchambuzi wa Matumizi ya Fedha za Umma kwenye sekta ya Maji zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) mwaka 2001 na 2002, pia na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2003 - 2005.
Akiwa mwenye uzoefu kwenye sekta zinazodhibitiwa na Ewura,  Ngamlagosi anatarajiwa kutekeleza majukumu na wajibu wake kama Mkurugenzi Mkuu wa Ewura kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu.

No comments: