Ikulu ya Zanzibar. |
Pamoja na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kusisitiza kwa wanasiasa katika kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, wajadili mambo mengine muhimu mbali na muundo wa Muungano, jana ilijidhihirisha kuwa hoja ya muundo huo, si tu nyeti kwa wanasiasa, bali pia kwa wasomi.
Tayari rasimu ya kwanza na ya pili ya Katiba Mpya, zimesisitiza wazi kuwa maoni ya Watanzania katika muundo wa Muungano, ni serikali tatu, lakini hawataki kuvunja muungano, huku mdau mkubwa wa Muungano, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikishikilia msimamo wa muundo wa serikali mbili.
Wiki iliyopita wakati viongozi wa vyama vya siasa walipokutana katika mkutano ulioitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alizungumzia muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Alisema muundo huo wa serikali mbili, unawezekana katika Katiba mpya tarajiwa, ilimradi kuwe na nchi moja. Alifafanua kuwa lazima pia kuwe na mamlaka kamili ya kusimamia sehemu zote mbili za Muungano na kuondoa mgongano wa kikatiba.
"Kwa kuondoa mgongano wa kikatiba ina maana ni lazima Katiba ya Zanzibar isitamke kuwa ni nchi yenye mamlaka kama ilivyo sasa," alisema Jaji Warioba.
Alitoa kauli hiyo, ingawa katika rasimu hizo za Katiba mpya zilizoandaliwa na Tume yake, wamesisitiza serikali tatu yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.
Juzi katika mkutano wa waandishi wa habari wa kutangaza mkutano wa jana wa wasomi ulioandaliwa na Utafiti ya Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP), mmoja wa watoa mada, Profesa Bonaventura Rutinwa, alionya kuhusu madhara ya Serikali tatu kwa Zanzibar.
Jana, Profesa Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye alianza pia kuzungumza mbele ya wasomi wenzake karibu 100, alisisitiza mfumo wa serikali tatu utaamsha kero kubwa zaidi ya zilizopo na zinaweza kuvunja Muungano.
"Sasa kwa kuwa Zanzibar tayari ina Katiba yake, inayotoa na kulinda haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Wazanzibari, huhitaji nguvu za kinabii kubashiri kuwa Katiba ya Tanganyika ikija, itatoa na kulinda haki za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa Watanganyika.
"Hii ikitokea, itasababisha wananchi kutoka Tanganyika wanaoishi Zanzibar na Wazanzibari wanaoishi Tanganyika kushindwa kudai haki zao za uraia kisheria," alionya Profesa Rutinwa.
Akisisitiza hadhari yake kwa muundo wa serikali tatu jana, Profesa Rutinwa alisema mfumo huo, unaweka rehani haki sawa za Watanzania, ambazo alidai hata sasa hazitolewi kwa usawa Zanzibar.
"Serikali mbili za sasa bado zina uwalakini kwa kuwa pamoja na kuwepo kwa Katiba ya Tanzania, bado Katiba ya Zanzibar inatoa haki kwa Wanzazibari zaidi kuliko Wabara Wabara wanakosa haki ya kuwa na ardhi wala kupiga kura Zanzibar lakini Wazanzibari wanafurahia haki zote za Tanzania Bara," alisema.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta, Kampasi ya Arusha, Profesa Ward Mavura, alisema njia pekee ya kumaliza matatizo yaliyopo katika Muungano ni mfumo wa serikali moja.
"Ikishaanzishwa serikali hiyo moja, ndipo zitakapoundwa serikali za majimbo kama ilivyo kwa Kenya na Marekani na Zanzibar badala ya kuwa nchi kama ilivyo sasa, iwe jimbo kama itakavyokuwa kwa majimbo mingine," alisema.
Majimbo hayo alitoa mfano kwamba kuanzishwe majimbo ya Kati, Kusini, Kaskazini, Magharibi na Mashariki.
Katika utekelezaji wa mfumo huo, serikali hiyo moja iwe ya Muungano, ambayo kazi yake itakuwa ni kushughulikia masuala yote ya Muungano. "Hii ya serikali tatu ni sawa na kuzidi kuwapatia haki zaidi Wazanzibari, je, majinbo mingine nayo yakidai?" Alihoji.
Profesa Humphrey Moshi kutoka Idara ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kuishusha hadhi Zanzibar kwa sasa na kuifanya jimbo, Tanzania imeshachelewa kwani tangu Muungano uasisiwe, Zanzibar iliachiwa ikawa na bendera, wimbo wa taifa, Rais, Baraza la Wawakilishi na Katiba yake.
"Na ndio kinachoendelea hadi sasa kwenye hii serikali tatu kwani itazidi kuipa nguvu Zanzibar, kama wasomi tujiulize kwa nini tunahitaji Muungano? Kwa kuwa kwa sasa tukubaliane tu kuwa ni ngumu kubadilisha mizizi ya Zanzibar tayari imeshakomaa," alisisitiza.
Sultan Rashid kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar alisema kwa hali halisi ilivyo sasa, serikali moja haitekelezeki, kwa kuwa matakwa ya Watanzania hayaendani na mfumo huo.
"Ukiuliza leo Wazanzibari wanataka nini, watakuambia wanataka Zanzibar iwe nchi na Watanganyika vivyo hivyo," alisema Sultan.
Hata hivyo, wakati wa kukusanya maoni ya Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilikusanya maoni tofauti Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Warioba, wakati wa kutafuta maoni, asilimia tano ya waliotoa maoni Tanzania Bara walitaka kusiwe na Muungano, asilimia 13 serikali moja, asilimia 24 serikali mbili na 61, serikali tatu.
Kwa upande wa Zanzibar, Jaji Warioba alisema asilimia 34, walitaka serikali mbili, 60 serikali ya mkataba, 23 serikali nne; yaani serikali ya Muungano, serikali ya Tanganyika, serikali ya Unguja na serikali ya Pemba.
"Hata sisi kwenye Tume tulikuwa kama ninyi, kuna wanaotaka serikali moja, wengine mbili, wengine tatu na mkataba, lakini hakuna aliyetaka serikali nne. Tulilazimika kuachana na mitazamo yetu na kuridhiana kwa kuja na mapendekezo ya serikali tatu," alisema.
Pamoja na maoni hayo, Sultan alisisitiza kuwa jambo la msingi kwa sasa ni kuandaliwa kwa Katiba yenye matakwa ya Watanzania wenyewe, isiyo na ushawishi wa wanasiasa, wasomi au kada yoyote, ili kuondokana na matatizo yanayoweza kujitokeza endapo wananchi hawatokubaliana nayo.
"Tuangalie mifano ya nchi za wenzetu, pale Katiba ilipochezewa na kuwekwa yale ambayo wananchi hawakuyataka, damu ilimwagika, sasa sisi kama wasomi tuhakikishe hilo hapa kwetu halitokei," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Esaurp, Profesa Ted Maliyamkono, alisema bado mjadala huo unaendelea leo, ambapo wasomi hao kwa pamoja watatoa na maazimio ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba bora.
"Pamoja na kwamba Bunge Maalumu la Katiba linaanza leo, tuna imani kuwa maoni na michango yetu tutakayoifikia, itafanyiwa kazi na wabunge wa Bunge hilo kwa faida ya Watanzania wote," alisema.
Awali, akifungua mjadala huo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka, alisema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kupatikana kwa Katiba imara, yenye mtazamo wa wananchi wote na itakayoleta mabadiliko.
No comments:
Post a Comment