KIWANJA CHA MWALIMU NYERERE CHAPIGWA DANADANA KINONDONI...

Hayati Mwalimu Nyerere.
Familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, imeendelea kupigwa chenga na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni, walikokwenda mara kadhaa kufuatilia haki ya kiwanja walichoachiwa na baba yao.

Kiwanja hicho inadaiwa na familia hiyo kuwa kimeporwa na kugawanywa katika miliki ya watu wawili na mporaji mmoja alianza ujenzi, ambao ulikuwa ukifanyika chini ya usimamizi wa mabaunsa huku mporaji huyo akiwa na bastola mkononi.
Taarifa zilizopo, zinaonesha kuwa kiwanja hicho kipo Msasani Beach karibu kabisa na makazi ya mjane wa Mwalimu, Mama Maria na kina namba 778.
Hata hivyo, baada ya kuporwa, inadaiwa  watuhumiwa wamefanya ujanja na kukigawa na kuwa viwili; kimoja kina namba 778 na kingine 782, wakati awali kilikuwa na namba moja 778.
Baada ya kutolewa habari ya kuporwa kwa kiwanja hicho kwa mara ya kwanza, kesho yake uongozi wa Wilaya ya Kinondoni uliingilia kati na kuzuia ujenzi katika kiwanja hicho, uliokuwa ukiendelea kwa mabavu.
"Tumefarijika sana, kimekuja kibali  saa tano asubuhi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya kwenda wa Mkuu wa Polisi Oysterbay kuzuia ujenzi uliokuwa ukiendelea," alisema mwanafamilia mmoja akishukuru gazeti hili kutoa habari hiyo, iliyosababisha uongozi wa Kinondoni kuchukua hatua haraka.
Hata hivyo, baada ya kibali hicho, wanafamilia hiyo waliambiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alikuwa na udhuru ameenda kwenye kozi ya wiki moja, hivyo amemuachia  Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Celestine Onditi aendelee na kikao hicho.
Mapema mwezi huu, mmoja wa wanafamilia hiyo (jina limehifadhiwa) alidai Katibu Tawala aliwaita kwa pamoja kwa ajili ya kikao hicho kilichokuwa kifanyike saa 4:00, asubuhi, lakini baada ya kufika alidai kuwa wamechelewa hivyo amemruhusu mlalamikiwa kuondoka kwa kuwa alifika mapema na wameshazungumza.
Mwandishi aliendelea kufuatilia, ambapo mwishoni mwa wiki iliyopita familia hiyo iliitwa tena kwa ajili ya kikao hicho, lakini walishangazwa badala ya kukutanishwa na DAS na mlalamikiwa, walikutanishwa na maofisa wengine wa ngazi ya chini.
Wakili wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Banzi, alilieleza gazeti hili kuwa kikao hicho kilitarajiwa kuendeshwa na DAS, lakini hakuwepo, badala yake kikao hicho kilihamishiwa kwa maofisa wengine ambao wanafamilia hiyo wanadai kutowatambua.
Aidha, Wakili Banzi alidai maofisa hao walianza kuwaonya na kuwalaumu kuhusu suala hilo kupelekwa katika vyombo vya habari.
"Walienda kwa ajili ya kikao na walitarajia kukutana na DAS, lakini walipofika haikuwa hivyo mambo yalikuwa tofauti walikutana na watu wengine kabisa ambao waliishia kuwalaumu tu," alidai Wakili huyo.
Mwanafamilia aliyezungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, alidai kuwa lawama walizopewa na maofisa hao ambao wao hawakuwatambua, walidai kwa nini wamepeleka  suala hilo kwenye vyombo vya habari, jambo linaloleta picha kuwa mtu huyo yuko juu ya Serikali.
"Walitulaumu kwa haya mambo kuonekana kwenye vyombo vya habari, lakini sisi tuliwaambia kuwa waandishi wa habari wameandika ukweli wa mambo yalivyo, wakatuonya kuwa tunatengeneza picha kuwa Serikali haipo," alisema.
Aliongeza baada ya kupewa lawama hizo, maofisa hao waliwaambia kuwa wao wasingeweza kuendesha kikao hicho badala yake wamsubiri Mkuu wa Wilaya kwani ndiye atakayewaita tena.
Mporaji aliyekuwa akijenga, katika kuonesha kiburi chake, inadaiwa alikuwa  akitamba kuwa hakuna mtu anayeweza kumfanya chochote huku  akihoji Mwalimu ni nani?
"Wanatamba hakuna mtu anayeweza kufanya chochote...wanafikia hatua ya kuhoji Nyerere ni nani, eti alikuwa zamani lakini kwa sasa hana chochote. Hizi kashfa zinatukera," alisema mtoa habari wetu, aliyetupa taarifa za uporaji huo.
Mtoa habari huyo alibainisha kuwa Jumanne kuamkia Jumatano ya Januari 22 mwaka huu saa 7 usiku, mtuhumiwa alifika katika eneo hilo na mabaunsa kama 30 ambao walikuwa akirandaranda katika maeneo hayo, ili kusimamia   umwagaji kifusi pamoja na kusawazisha, huku mmoja wa waporaji hao (jina tunalo) akiwa ameshikilia bastola mkononi.

No comments: