Dk William Mgimwa (kushoto) na mwanae, Godfrey. |
Godfrey Mgimwa (32) anaelekea kurithishwa viatu vya marehemu baba yake, Dk Mgimwa katika Jimbo la Kalenga, baada ya juzi kuibuka kidedea katika kura hizo, takribani mwezi mmoja tu tangu baba yake afariki dunia Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.
Wajumbe 708 kati ya wajumbe halali 816 wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kalenga kupitia chama hicho, waliwasikiliza na kuwapigia kura wagombea hao katika uchaguzi huo
uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwembetogwa, mjini Iringa.
Upigaji kura ulianza saa tisa alasiri baada ya kila mgombea
kupata fursa ya kujieleza na kuomba kura, na matokeo yalitangazwa saa tatu usiku baada ya uhesabuji kura kukamilika.
Mgimwa anayepigiwa 'upatu' wa kushinda katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo utakaofanyika Machi 16, mwaka huu, alishinda kwa kuzoa kura 348 za maoni.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa kura hizo, Joseph Muhumba alisema Mgimwa alifuatiwa kwa mbali na Mkurugenzi wa Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga aliyepata kura 170.
Wengine na kura chache walizoambulia kwenye mabano ni Thomas Mwikuka (2), Edward Mtakimo (3), Bryson Kalinga (7), Williama Pangamila (8), Peter Mtisi (33), Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtasiwa (42) na Gabriel Kalinga (90).
Kabla ya kura hizo kupigwa, minongÕono kutoka kwa baadhi ya wajumbe ziliashiria kuwepo kwa ushindani mkubwa kati ya Kiswaga, Mtasiwa na Kalinga.
Hata hivyo Mgimwa alitumia vyema nafasi aliyopewa kujieleza wakati akiomba kura hali inayoelezwa na wajumbe wengi kubadili upepo katika kura hizo.
Bila kumtaja marehemu baba yake, Mgimwa alisema; "Mimi ni mwenzenu, mkazi wa Kalenga niliyebahatika kupata elimu nzuri pamoja na kwamba kiumri bado ni mdogo."
AlisemaÊ baada ya kumaliza elimu ya sekondari hapa nchini, alibahatika kwenda nchini Uingereza alikopata shahada ya kwanza na ya pili katika fani ya biashara na masoko.
"Baada ya kumaliza mwaka 2010 nilirejea nchini na kuajiriwa na benki ya Stanbic Makao Makuu ninakofanya kazi hadi nakuja kuwaomba mnipigie kura ili niwawakilishe katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga," alisema.
Alisema kwa kupitia Ilani ya CCM, atajikita katika kushughulikia kero zinazowahusu wananchi wa jimbo hilo huku kipaumbele chake kikuu kikiwa ni elimu.
Kabla ya kuwashukuru wajumbe kwa kumchagua katika kura hizo za maoni, wagombea wengine wote walikubali matokeo na kuahidi kushirikiana naye katika hatua zote muhimu zitakazoihakikishia CCM ushindi.
Endapo atapitishwa na vikao vya juu vya CCM, Mgimwa anatarajiwa kumenyana na wagombea wa vyama vingine vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitakachofanya kura zake za maoni Jumatano ya Februari 12.
Wakati akifungua mkutano wa kura hizo za maoni, Kaimu Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga aliwataka wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM kuwa wamoja mara baada ya kura hizo.
"Uzoefu unaonesha kura za maoni zimekuwa zikikigawa chama kwenye baadhi ya maeneo, tuachane na dhana ya kutoshindwa katika chaguzi zetu za ndani,"alisema.
Alisema wagombea wakionesha mshikamano baada ya kura za maoni itazidi kuimarisha chama na kukiweka katika mazingira salama ya kushinda chaguzi zijazo.
Taarifa ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka, inaonesha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepanga tarehe ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kuwa ni Machi 16, mwaka huu.
Kwa upande wa wagombea kutoka katika vyama vitakavyoshiriki, taarifa hiyo ilieleza kuwa fomu za uteuzi zitatolewa Februari 9 hadi 18 mwaka huu.
Uteuzi wa wagombea utafanyika Februari 18 na kampeni za uchaguzi huo zitaanza Februari 19 hadi Machi 15 mara baada ya uteuzi.
Aidha, daftari la wapiga kura litakalotumika katika uchaguzi huo ni lile lililotumika mwaka 2010 linaloonesha jimbo hilo lina wapiga kura zaidi ya 85,000.
No comments:
Post a Comment