HUKUMU YA JENGO LA GHOROFA 18 KARIBU NA IKULU KUTOLEWA LEO...

Jengo hilo lenye ghorofa 18 lililoko jijini Dar es Salaam.
Hukumu ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji wa kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 18 karibu na Ikulu Dar es Salaam, inayowakabili vigogo wawili wa Wakala wa Ujenzi, inatarajiwa kutolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Hakimu wa mahakama hiyo, Sundi Fimbo, ndiye anayetarajiwa kutoa  hukumu ya kesi hiyo iliyofunguliwa   mwaka jana baada ya kupitia ushahidi na vielelezo mbalimbali vilivyotolewa na pande zote mbili mahakamani hapo kwa nyakati tofauti
Washitakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na aliyekuwa Msanifu Mkuu wake, Richard Maliyaga.
Kimweri na Maliyaga wanakabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi, katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja namba 45 mtaa wa Chimara.
Awali akijitetea mahakamani hapo, Maliyaga alidai kuwa Mkurugenzi wa Miliki wa Wakala, Charles Makungu, ndiye aliyekuwa na uamuzi wa mwisho wa kutoa kibali cha ujenzi na kupeleka barua katika halmashauri husika na kwa waleta maombi.
Akiongozwa na Wakili Majura Magafu, Maliyaga alidai alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kutoa Vibali na walipopata ombi la ujenzi huo, walipitia michoro na baada ya kuona ipo sawa walisaini kibali na kupeleka kwa Makungu.
Alidai kuwa awali aliandika barua akipendekeza ofisi ya Makungu iombe kibali kutoka Halmashauri ya Ilala, lakini hakupata majibu hadi alipopewa maelekezo kutoka katika Kamati inayoshughulikia miradi ya ubia, kuwa watoe kibali hicho.
Alidai alikataa kutoa kibali hicho lakini baada ya wanakamati kujadili, walikubali kufuata maelekezo hayo na kutoa kibali hicho.
"Sisi hatukuhusika kutoa uamuzi wa mradi huu, mimi nimeonewa kwa sababu sijanufaika na sikutumia madaraka yangu vibaya, nashangaa kwanini watu kutoka katika kamati yetu au ile ya miradi ya ubia hawajaletwa mahakamani," alidai Maliyaga.
Katika utetezi wake pia Kimweri alidai kuwa amefunguliwa kesi hiyo kwa kuwa alikuwa na ugomvi na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli baada ya kumchafua kwenye vyombo vya habari na ndiyo sababu ya kupewa shutuma hizo.
Alidai ugomvi huo ulitokana na mchakato wa uuzwaji wa nyumba za Serikali, ambapo yeye alikataa kusaini mkataba wa kumuuzia nyumba mwanafunzi kwa sababu hakustahili ndipo Magufuli alipodhani kuwa alitoa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari.

No comments: