MSHITAKIWA WA KWANZA KESI YA UTOROSHAJI TWIGA AUGUA GHAFLA...

Twiga.
Kesi utoroshwaji wa twiga kwenda Uarabuni, imekwama baada ya mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Kamran Ahmed, kuugua ghafla muda mfupi kabla ya kufika mahakamani hapo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi, jana ililazimika kuahirisha kesi hiyo baada Wakili wa mshitakiwa huyo, Edmund Ngemela, kuieleza mahakama hiyo kwamba sukari ya mshitakiwa huyo ilipanda na kusababisha ashindwe kufika mahakamani kuendelea na kesi inayomkabili.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Simoni Kobelo na mawakili wa pande zote mbili, Ngemela alidai hali ya afya ya mteja wake, ilisababisha ashindwe kufika mahakamani hapo.
"Mheshimiwa Hakimu kesi hii ilikuja kwa ajili ya kuendelea na mashahidi upande wa mashitaka, lakini niiombe mahakama yako tukufu, iahirishe kwani mteja wangu, sukari imepanda kuliko kiwango cha kawaida," alisema.
Katika kesi hiyo iliyozungumzwa katika mahakama ya ndani, tofauti na juzi ambapo ilisikilizwa katika mahakama ya wazi, mawakili wa Serikali hawakuwa na pingamizi dhidi ya maombi hayo na kutaka mahakama kufuata taratibu zake.
Kesi hiyo ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi ambapo upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili Evetha Mushi, Joseph Maugo na Steven Mwanasenjele, ulifika kwa ajili ya kuongoza mashahidi
wao kuendelea na ushahidi katika kesi hiyo.
Tayari upande wa mashitaka umeleta mashahidi 21 na 
jana ilikua ni mwendelezo wa mashahidi wake kufika mahakamani hapo.
Kutokana na maombi hayo, Hakimu Kobelo aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 21, 24 na 25 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari nje ya mahakama, Wakili Ngemela alisema mteja wake alimuacha nyumbani kwake asubuhi, akijiandaa kwenda hospitali kutazama zaidi afya yake.
Hata hivyo kesi hiyo ambayo ilipangwa kusikilizwa kuanzia saa 3.00 asubuhi katika mahakama ya wazi,  wanahabari walijikuta wakisubiri hadi saa 4.55 asubuhi bila kufahamu kilichoendelea hadi walipotaarifiwa kesi inakaribia kuahirishwa katika mahakama ya ndani.
Juzi shahidi wa 20, Robert Nyanda alielezea  alivyopokea maelekezo kutoka kwa bosi wake Rosemary Israel ya kuandaa vifaa vya kuinua vitu vizito kwa ajili ya kupakia wanyama hao katika ndege ya Qatar.
Aidha, shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa siku ya tukio wanyama hao walipakiwa katika ndege hiyo saa nane usiku na waliletwa uwanjani hapo na lori aina ya Fuso pamoja na vijana maalumu kwa ajili ya kusaidia upakiaji wake katika ndege.

No comments: