Kikao cha Bunge Maalumu mjini Dodoma. |
Vizingiti hivyo vimetangazwa jana katika taarifa iliyoandaliwa na Kamati Maalumu ya kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu aliwasilisha taarifa hiyo pamoja na Rasimu mpya baada ya kazi ya siku sita iliyojumuisha wajumbe 20.
Rasimu mpya ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, imepiga marufuku Mwenyekiti au Makamu wake, kuhudhuria kikao cha kikundi chochote kinachowakilishwa bungeni.
Kumekuwapo na desturi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti, ambao wanatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huhudhuria vikao vya chama vya wabunge hao.
Aidha katika Bunge Maalumu inatarajiwa wajumbe ambao ni wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao ni wanachama wa CCM, watakuwa wakikutana mara kwa mara kukitokea ubishani.
Mbali na wajumbe hao, pia wajumbe ambao ni wawakilishi na wabunge wanachama wa vyama vya upinzani, ambao wameungana katika suala la Katiba mpya, nao wanatarajiwa kukutana mara kwa mara wakati wa Bunge hilo.
Aidha katika kudhibiti ushawishi wa kundi analotoka katika kupitisha vipengele vinavyoshindaniwa katika Katiba hiyo, rasimu hiyo imetamka kuwa Mwenyekiti na Makamu wake, hawatafungwa na msimamo au makubaliano yaliyofikiwa na kikao hicho.
Kanuni hiyo imewekwa huku wajumbe wanachama wa CCM, wakiwa wameshatangaza msimamo wao katika muundo wa serikali kuwa ni serikali mbili, huku wanachama kutoka vyama vya upinzani waking’ang’ania serikali tatu.
Rasimu hiyo pia inapendekeza kuondolewa madarakani kwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Mbali na hilo, pia mgombea yeyote wa nafasi ya Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti hataruhusiwa kujitoa baada ya uteuzi kufanywa.
Katika kumwondoa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti, Kanuni inapendekeza Mjumbe mwenye hoja ya aina hiyo, atapaswa kuiwasilisha kwa maandishi kwa Katibu wa Bunge, akieleza sababu za kutaka kuleta hoja hiyo.
Baada ya kuipokea, Katibu ataipeleka kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu kuijadili, na ikiridhika kuwa zipo tuhuma mahsusi dhidi ya mhusika, itaidhinisha hoja hiyo ipelekwe bungeni kwa uamuzi.
“Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti atakuwa ameondolewa madarakani endapo zitapigwa kura za siri na kupata wingi wa kura zilizopigwa,” ilieleza Kamati.
Endapo nafasi ya Mwenyekiti itakuwa wazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo kifo, kujiuzulu au kupigiwa kura ya kutokuwa na imani, nafasi yake itajazwa katika siku zisizozidi mbili.
Kamati hiyo ya Profesa Mahalu pia imekuja na mapendekezo ya kuwa na Kamati 16, badala ya 20 za awali, huku ikija na Kamati mpya ya Maridhiano.
Kwa mujibu wao, Kamati ya Maridhiano itakuwa na majukumu ya shughuli zinazohusu maridhiano au mwafaka juu ya mambo yanayobishaniwa na wajumbe wa Bunge Maalumu.
Nyingine ni kutoa taarifa katika Bunge Maalumu kuhusu mwafaka uliofikiwa juu ya mambo yaliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo.
Kabla ya kuanza kwa Bunge Maalumu, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipendekeza wajumbe wa Bunge hilo kupitisha vifungu na katiba hiyo kwa kutumia maridhiano badala ya kura.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kama rasimu ya Katiba ikipitishwa kwa kura, itakuwa katika hatari ya kupingwa kuanzia siku iliyopitishwa.
Aidha, Kamati hiyo inapendekeza utaratibu wa kura ya siri kutumika katika kupitisha hoja ya Kamati, na pia katika kupitisha masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara, tofauti na Rasimu ya Kanuni ya awali.
“Mambo yote yatakayojadiliwa na Kamati ya Bunge Maalumu yataamuliwa kwa theluthi mbili ya wajumbe wa Kamati waliohudhuria na kupiga kura,” ilifafanua Rasimu mpya ya Kanuni za Bunge.
Katika Rasimu ya awali, ilipendekeza kura ya mwisho ya kuamua Rasimu ya Katiba ndiyo iamuliwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wa Zanzibar.
Aidha, kila Kamati ya Bunge Maalumu itajadili Rasimu ya Katiba kwa mujibu wa mgawanyo wa Sura za Rasimu ya Katiba zinazofanana kwa Kamati hizo uliowekwa na Kanuni kwa muda usiozidi siku mbili.
Katika majadiliano, mjumbe yeyote hataruhusiwa kutoa salamu, shukrani au pongezi wakati wa kuchangia hoja au mjadala katika Bunge Maalumu na ikitokea hivyo, Mwenyekiti atamwamuru kukaa chini.
Rasimu mpya pia inapendekeza utaratibu utakaoruhusu taarifa ya maoni kinzani kuandaliwa na kuwasilishwa katika Bunge Maalumu, ili kuwezesha mawazo ya wajumbe wachache wenye mtazamo tofauti yasikike.
Kwa mujibu wa Rasimu, Taarifa kinzani ni taarifa iliyoandaliwa na idadi ndogo ya wajumbe wachache wa Kamati ambao hawakubaliani na maoni ya wajumbe walio wengi wa Kamati.
Wakati wa kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba, Kanuni inapendekeza kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu wasiruhusiwe kuomba ufafanuzi na pia kutoa hoja za ‘kuhusu utaratibu’ au ‘Mwongozo wa Mwenyekiti.’
“Lengo la pendekezo hilo ni kumwezesha Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa mujibu wa Sheria,” alisema Profesa Mahalu.
Kanuni hiyo ya kina Profesa Mahalu pia imeendelea kuruhusu kuwapo kwa vikao vya faragha vya Kamati za Bunge Maalumu, kama ilivyokuwa Rasimu ya awali.
Kuhusu amani na utulivu bungeni, Kanuni mpya inapendekeza kupunguza adhabu ya kifungo cha siku 10 hadi kuwa vikao vitatu kwa Mjumbe yeyote atakayevunja au kujaribu kuvunja amani na utulivu kwa kutumia nguvu au mabavu ndani ya Ukumbi.
Aidha, imesema lugha rasmi itakayotumika katika majadiliano ni Kiswahili, na kuainisha mavazi rasmi yatakayovaliwa na wajumbe wa Bunge hilo.
Kamati ya Profesa Mahalu iliyokuwa na kazi ya kupitia Rasimu ya awali iliyoandaliwa na Sekretarieti, ilijumuisha wajumbe 20, 10 kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hao ni Mgeni Hassan Juma (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti), Magdalena Rwebangira (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti), Ismail Jussa Ladhu, Jaji Frederick Werema, Tundu Lissu, Profesa Abdul Sheriff, Nakazael Tenga, Adila Hilal Vuai, George Simbachawene.
Wengine ni Tulia Ackson, Evod Mmanda, Angella Kairuki, Honoratha Chitanda, Peter Mziray, Abubakar Khamis Bakar, Ussi Jecha Simai, Amon Mpanju, Elizabeth Minde na Othman Masoud Othman.
No comments:
Post a Comment