Mama huyo akiwa na mwanae chooni humo wanamoishi. |
Hali hiyo imekuwa ikitumiwa na mwanamama Aziza Mohammed ambaye kutokana na taharuki ya upepo na mvua hiyo alilazimika kukimbilia katika choo chake cha kisasa ambacho alijenga kikiwa imara kuliko hata nyumba ya kuishi siku chache kabla ya tukio.
Baada ya tufani hilo kutulia na makundi mbalimbali ya watu wakiwemo viongozi kuanza kutembelea tukio ndipo alipobaini kuwa kukaa kwake chooni kunaweza kumpatia misaada na kuamua kufanya hivyo kwa kila anapopewa taarifa ya ujio wa makundi hayo.
Tofauti na wenzake waliopata maafa ambao waliombewa makazi ama kukaribishwa kwa majirani, lakiniĆ kwa Aziza ilikuwa ni patashika kukubali kufanya hivyo mpaka pale viongozi wa kata na kijiji pamoja na maofisa wa maendeleo ya jamii walipoenda kumshawishi na kukubali kuhama.
Hata hivyo, hakuweza kuridhika baada ya kubaini kuwa atapatiwa msaada wa bati wa kutosheleza vyumba viwili ambavyo vitajengwa kwa kununuliwa tofali za kuchoma na wasamaria wema na hivyo kukubali kurudishwa na baadhi ya waandishi wa habari ili kwenda kupigwa picha kule chooni akichukuliwa kutoka kule alikopewa hifadhi.
Hatua hiyo ilijitokeza baada ya kutoridhika na vyumba viwili na kuwaeleza waandishi wa habari hao kuwa mkoa na wilaya umeshindwa kumsaidia na hivyo anamsubiri Waziri mkuu Mizengo Pinda.
"Ni kweli ilikuwa ni patashika kumhamisha huyo mama kutokana na mtazamo wake kwamba akiishi hapo chooni baada ya nyumba yake kuezuliwa paa atapata misaada, lakini viongozi wa kitongoji, kijiji na wa maendeleo ya jamii walimuelimisha baadaye alikubali, lakini cha ajabu leo(juzi) waandishi wa habari hao wamemchukua na kumrudisha kule chooni ili kupata picha," alisema mmoja ya viongozi wa kitongoji.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga ameeleza kuwa serikali wilayani humo kwa kushirikiana na Mbunge wa jimbo la Hai, Freeman Mbowe wameweka mazingira ya dharura ya kusaidia kaya ambazo makazi yao yapo katika hali mbaya yakiwemo ya Aziza na wengine wengi kwa kutenga fedha za kununua matofali ya kuchoma.
Makunga alieleza kuwa pamoja na kuwepo kwa msaada wa mabati 200 kutoka kwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP kupitia Bonite Bottlers, lakini ni vigumu kuezeka katika nyumba nyingi kutokana na kukosa uimara ikiwemo aliyokuwa akiishi Aziza hivyo wanajipanga kumnunulia tofali imara za kuchoma za vyumba viwili.
Lakini pia alisema kuwa msaada kama huo utapelekwa kwa mzee aliyemtaja kwa jina moja la mzee Omar wa kitongoji cha Kijiweni ambaye hana msaada pamoja na mama mjane wa kijiji cha Kikavu Chini ambaye atapatiwa bati lakini kijiji kimekubali kufanya harambe ya kumsaidia kukamilisha nyumba yake.
Makunga alieleza kuwa kutokana na uchache wa msaada, hasa bati bado uchanganuzi unafanyika ili kuweza kuzigawa kwa wale ambao wana hali mbaya zaidi.
No comments:
Post a Comment