Anne Makinda. |
Wakati Makinda akitoa ushauri huo kwa wajumbe wanawake wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa upande wake Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake, Anna Abdalah amesema wanaosema posho ya Sh 300,000 kwa siku haitoshi wana sababu zao.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa kwenye semina iliyoandaliwa na Tanzania Women Cross Party Platform kwa ajili ya wajumbe wanawake wa Bunge Maalumu linaloendelea mjini hapa.
Ingawa Makinda hakulenga moja kwa moja kuzungumzia sakata la posho kwa wajumbe wa Bunge Maalumu ambalo limeibua mjadala kwenye jamii, baada ya baadhi ya wabunge kudai Sh 300,000 kwa siku hazitoshi, alisema kasoro ya wabunge wengi wa Tanzania ni kuamini kwamba wanakwenda kutajirikia bungeni.
"Na sisi wenyewe tushughulikeÉutakuta wanadai bahasha za spika, bahasha za spika, zitaisha baada ya miaka mitano na wanaondoka mikono mitupu," alisema.
Alisema siku moja, waliwaalika wabunge kutoka Zimbabwe ambao waliwapa changamoto kubwa ya kuhakikisha wanakuwa na miradi ya kuwaingizia kipato kuepuka kutegemea bungeni.
"Wakasema (Wazimbabwe) wewe mwenyekiti una kitu gani unachofanya, hakuna kwa hiyo tunapokwenda kwenye kugombea hatuna pesa kwa sababu hatuna kitu," alisema.
Aliendelea kusema, "Usije hapa (bungeni) kwa sababu kuna pesa, njoo hapa kama mwakilishi. Fanya shughuli zako. Hii nasema kwa sababu kwenu ninyi (wajumbe wa Bunge Maalumu) ndiyo mtakaokuwa wagombea mwaka 2015. Anza kuangalia kwenye kazi zenu. Vitu gani vinaweza kukupa mapato zaidi, unaweza kufanya nini kusudi ukija hapa usiwe unakuja 'purely' unategemea hapa," alisema Makinda.
Aliendelea kusema, "Hapa kukiwa na matatizo, kesho unaondoka huna kitu. Hii ndiyo kasoro ya Tanzania. Wabunge wa Tanzania ugomvi wetu ni huo. Mtu anatoka anakotoka anaamini anakuja kutajirika. Hakuna hapa kutajirika."
Makinda aliendelea kusema, "Hapa tunawapa mikopo (wabunge) wanakopa hapa, lakini na wengine wanauza , wanatumia hela hizo halafu wanabaki masikini. Baada ya miaka, miezi miwili baada ya uchaguzi, kifo. Anatoka mtu ziro," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, anataka kuanzisha masomo ya ujasiriamali kwa vijana ambao hawana kitu. Alitaka wajumbe hao wa bunge maalumu wanaotaka kugombea katika uchaguzi wajiandae kwa hilo.
Makinda ambaye katika semina hiyo, aliweka wazi kwamba hatagombea, aliwaambia wajumbe, "sisi wenzenu tumeshamaliza wakati wetu hatutasimama tunawaachia nyie."
Akizungumzia wanaosema posho haitoshi, Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake, Abdallah wakati akimkaribisha Makinda kufungua semina, alisema wanaosema hivyo wanalo lao jambo.
Aliwataka wajumbe hao wa Bunge Maalumu kutambua kwamba wamekuja kuangalia maslahi ya Watanzania na si posho.
"Wakituongezea, siyo neno. Sisi hatukuja kujaza idadi, tumekuja kuonesha walipo wanawake hakiharibiki kitu," alisema Abdallah.
Wakati huo huo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alimwambia mwandishi jana kwamba kamati iliyoteuliwa kushughulikia suala la posho inaendelea na vikao vyake kabla ya kuwasiliana na serikali.
Kwa mujibu wa Dk Kashililah, jana walikuwa na kikao asubuhi na jioni. Hata hivyo hakuzungumzia zaidi ni nini itakwenda kuzungumza na serikali zaidi ya kusema vikao vitakapomalizika, ndipo anaweza kuzungumzia.
Kamati hiyo ya watu sita iliundwa juzi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho. Wajumbe wake ni Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenista Mhagama, Mohamed Aboud Mohamed, Asha Bakari Makame na William Lukuvi.
Kificho alihakikishia wajumbe wa Bunge Maalumu kwamba timu hiyo inayofanya kazi kama kamati ya uongozi, itashauri na hatimaye serikali ione umuhimu wa kufanyia kazi suala hilo la posho ambalo wabunge wanalalamika kwamba Sh 300,000 walizopangiwa kwa siku hazitoshi.
Vinara waanzilishi wa madai kwamba posho haitoshi ni Richard Ndassa ambaye ni Mbunge wa Sumve.
Akizungumza bungeni hivi karibuni, alisema kiasi hicho cha posho kwa siku kilichotolewa, kulingana na hadhi ya wabunge, hakitoshelezi matumizi kwa ajili ya hoteli, chakula, usafiri na malipo kwa madereva wao.
Katika hatua nyingine, Chama cha Walimu (CWT) katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara, kimewashangaa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba la kutaka kuongezewa posho wakidai Sh 300,000 ni ndogo kwa siku na kuwataka wasiotaka posho hiyo waondoke.
Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Bunda, Francis Ruhumbika alisema kuwa kama wajumbe hao hawataki ni bora wakarudi majumbani mwao na Rais ateue wengine wanaoweza kufanya kazi hiyo kwa maslahi ya umma hata kwa posho ya Sh 40,000 kwa siku.
"Wanasema kuwa hizo Sh 300,000 ni ndogo eti kutokana na hali ya maisha ya Dodoma, mbona hapo Dodoma kuna walimu wetu wanaolipwa mshahara chini ya 300,000 na wanaishi kama hawataki waache twende sisi nikiwemo mimi nilipwe hata Sh 40,000 tu nikafanye kazi hiyo ya umma," alisema.
Kutoka Tabora, baadhi ya wananchi wamelaani vikali kitendo cha baadhi ya wabunge wa Bunge la Katiba, kutaka kuongezewa posho na kumwomba Rais wa Jakaya Kikwete, kulivunja bunge hilo kwa maslahi ya umma.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora mmoja wa wananchi hao, Jonson Kisamba, alisema kitendo cha baadhi ya wabunge hao kuomba nyongeza ya posho ni kielelezo tosha kwamba wameenda hapo kuvuna pesa siyo kutunga katiba kwa ajili ya mustakabali wanchi.
Kisamba alisema wabunge hao wamekwenda hapo kujadili mambo ya katiba ya nchi na siyo kujadili misingi ya nchi ambayo ni uchumi, wala kuvunja muungano hivyo akapendekeza bunge hilo livuinjwe hadi rais atakapotangaza badaye.
No comments:
Post a Comment