Kanisa la Anglikana Mkunazini, Zanzibar. |
Ofisa Mwandamizi wa Kanisa la Anglikana la Mkunazini, Father Emmanuel Masoud, alisema jana kuwa watu waliosababisha milipuko hiyo walikuwa na lengo la kuvuruga amani na kutisha Wakristo wa hapa.
“Wapo watu wanasema hayo ni matukio ya kawaida yanayofanywa katika makanisa na migahawa ya kitalii...lengo lake ni sehemu ya hujuma na hakuna lingine,” alisema.
Kwa mfano, Masoud alisema wiki iliyopita Jumapili, Kanisa la Assemblies of God la Kijitoupele, lilishambuliwa na watu wasiojulikana na hadi jana hakukuwa na taarifa yoyote iliyotolewa na vyombo husika vya usalama.
“Narudia na kusema haya ni matukio ya makusudi ambayo yamelenga kudhalilisha Wakristo wasifanye ibada zao na kuathiri biashara ya utalii,” alisema Masoud akizungumza na gazeti hili katika eneo la Kanisa la Mkunazini.
Hata hivyo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani, kwamba matukio hayo ni ya kawaida na yasihusishwe na mwelekeo wa kisiasa au kidini.
Masoud alisema ulinzi umeimarishwa eneo la Kanisa la Anglikana, ambako kabla ya kuingia ndani ya eneo la Kanisa, wageni wanaotembelea hapo wanakaguliwa kwa vyombo vya kisasa.
Alisema shughuli zimerudi kama kawaida, ambapo idadi kubwa ya watalii wanaotembelea Kanisa hilo kongwe nchini, walionekana wakipata maelezo ya historia ya Kanisa hilo.
“Tunafanya upekuzi wa wageni wanaoingia katika eneo la Kanisa hili kwa ajili ya usalama zaidi wakiwamo wenyeji na watalii,” alisema ofisa wa ukaguzi wa Kanisa hilo.
Jeshi la Polisi lilisema litaanza kurudisha huduma za ulinzi katika majengo ya ibada na hasa makanisa ambayo yanaonekana kwamba yanalengwa na hujuma.
“Tumeanza kurudisha huduma za ulinzi wa Polisi kutokana na kujirudia matukio ya uhalifu na kushambuliwa kwa makanisa,” alisema ofisa wa Jeshi la Polisi ambaye hakupenda kutaja jina lake.
Juzi watu wasiojulikana walisababisha milipuko miwili nje ya lango kuu la kuingilia Kanisa hilo ambayo hata hivyo haikusababisha madhara makubwa.
Eneo la nje ya Kanisa ambalo huegeshwa magari, kimewekwa kibao kinachopiga marufuku kuegesha magari eneo hilo kwa usalama.
No comments:
Post a Comment