BUNGE LA KATIBA LAWEKWA NJIAPANDA KUHUSU KURA YA SIRI...

Kifungo cha kura ya siri katika Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, kimeliweka Bunge njia panda baada ya wajumbe bila kujali vyama na makundi, kugawanyika.

Chini ya kanuni zilizopendekezwa, utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo kutoa swali la kulihoji, utakuwa ni kwa kura ya siri. 
Wakati wa kupata uamuzi wa Bunge kuhusu kupitisha Rasimu ya Katiba, Bunge litapiga kura ya siri ambayo kwa madhumuni ya kanuni, itaitwa kura ya mwisho.
Baadhi ya wajumbe wa vyama vya upinzani, makundi maalumu na wachache wa CCM, waliunga mkono kura hiyo kwa hoja mbalimbali, ikiwamo ya kuwapa uhuru wajumbe wakati wa kufanya uamuzi.
Waliopinga wengi wao wametoka CCM, na walitoa hoja mbalimbali, ukiwamo umuhimu wa kura ya wazi kuzuia wajumbe wasisaliti wananchi waliowatuma na waliotoa hoja katika Rasimu ya Katiba mpya.
Kutokana na mkanganyiko huo, mjumbe Anne Kilango-Malecela, alishauri ipigwe kura ya siri kuamua suala hilo.
Katika hoja yake, Kilango alisema yapo makundi mawili; moja likiunga mkono mapendekezo kwenye Rasimu yanayotaka kura iwe ya siri na wengine wakipinga kwa kutaka iwe ya wazi.
Juzi mjadala ulipoanza,  baadhi ya wajumbe walitaka itumike kura ya siri huku wengine wakitaka kura ya wazi.
Lakini jana baadhi ya wabunge, Esther Bulaya na Profesa Juma Kapuya, waliunga mkono upigaji kura ya wazi.
“Kuhusu hili suala la kura, walioongea kuhusu kura za siri,  nimemsikia   Lipumba (Profesa Ibrahim) leo asubuhi, akanishawishi. 
“Nimemsikiliza Shehe Kundecha, amezungumza vizuri sana. Mazungumzo yake yana ushawishi.  Lakini Mwenyekiti, wanaozungumza kuhusu kura ya wazi, ukiwasikiliza vizuri nao wana ushawishi.
“Sasa nakuomba Mwenyekiti, hakuna kitu kizuri kama kuwapa wengi (anakatizwa na sauti za kuguna na kushangilia), ifike mahala hili suala tulipigie kura ya siri…kwa sababu yote mawili yakizungumzwa yana mvuto, tulipigie kura ya siri na watakaokuwa wengi turidhiane, kwamba tufuate mkondo huo,” alisema Kilango.
Kwa upande wake, Bulaya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, alipendekeza kura ya siri akisema ni vigumu kupima uzalendo kwa kupiga kura ya wazi.
“Ndiyo, utaratibu niliouzoea hata kwenye chama changu,  sijawahi kuchagua Mwenyekiti kwa kura ya wazi. Katika hili tuwe wakweli, nitasema kweli fitna kwangu ni mwiko. Hapa tunapitisha Katiba ya Watanzania nitapiga kura mimi kama Ester.
“Tusitengeneze mazingira ya kuanza kufarakana, mazingira ya kumbana mtu kisirisiri, haiwezekani,” alisema Bulaya.
Profesa Kapuya  katika kuchangia, alisema, “tutakapopiga kura ya siri, tutatoka hapa tumeimarika. Nazungumzia hapa ni umiliki wa Katiba,
inapaswa kuwa ya sisi sote tusitoke hapa tunasema ni Katiba ya kundi fulani. Naamini kura ya siri ndiyo itatufikisha tunakotaka kwenda.”
Shehe Kundecha alisema inabidi ieleweke kuwa upo uhuru wa mtu na uwazi wa mambo. Alihadharisha kwamba panahitajika mazingira yatakayowezesha hadi mwisho wa Bunge, wote wanakuwa kitu kimoja.
Alisema kura ya siri ndiyo itakayowaacha wakiwa na mshikamano. Alisisitiza kuwa kura ibaki kuwa ya siri na uwazi ubaki kwenye kuhesabu kura zitakazopigwa.
Mchungaji Christopher Mtikila alisema ustaarabu wa kidemokrasia, unaozingatia haki za binadamu za kila mjumbe, unakataa vikundi vinavyohujumu uhuru wa wananchi.
“Mwenyekiti tumekuchagua kwa kura ya siri. Si kwamba tulikuwa wajinga kuliko wenzetu.  Hapana,  ni ustaarabu halisi wa kidemokrasia. Kwa sababu ya uhuru wa maoni na kujieleza,  kuzungumzia habari ya ujasiri, sijaona nchi hii mwenye ujasiri kama mimi,” alisababisha kicheko.
Aliendelea: “Lakini kwa ajili ya haki na utu wangu, sipendi jirani yangu niliyekaa naye aende aseme Mchungaji Mtikila alipiga kura kumkataa mtu.
“Ni sawa na anayetoa taarifa Polisi, halafu polisi anaondoka anasema Mchungaji Mtikila ndiye aliyeleta habari hizi, halafu mimi nakwenda nakuwa wa kuwindwa barabarani.”
Philemon Ndesamburo, alionya juu ya ushabiki wa mambo ya vyama na kuasa wajumbe wenzake kuachana na ushabiki ndani ya Bunge Maalumu.
Pauline Gekul.  alisema chanzo  cha tofauti hizo, ni msimamo wa wajumbe juu ya aina ya Serikali inayotakiwa, kutokana na kuwapo kundi linalotaka serikali mbili na wengine serikali tatu.
“Kuna watu wanaugulia, ni waumini wa Tanganyika, lakini wanafungwa na msimamo wa chama chao,” alisema Gekul.
Hata hivyo, mjumbe Stephen Wassira, alisema vyama vyote vina misimamo yao.
Alisema kama jamii, wajumbe wanapaswa kukaa pamoja, kushauriana kwa hoja na mwisho wakubaliane, kuwa hiyo ndiyo Katiba na  watakuwa wanadanganyana wakisema kuna wenye msimamo.
“Wewe ulikujaje bila msimamo?” Alihoji Wassira na kusisitiza kuwa kila kundi, wakiwamo wavuvi, wanawake, wakulima, limekuja na msimamo na wengine wanapiga kampeni wazi.
Wengine waliochangia juzi wakitaka kura ya wazi ni pamoja na Profesa Anna Tibaijuka, aliyesema anapata wasiwasi na demokrasia nchini iwapo watu wanahofu kufukuzwa na vyama kwa kusema ukweli kupitia kura ya wazi.
Profesa Tibaijuka alitoa uzoefu wake, kwamba mabunge mengi duniani ukiwamo Umoja wa Mataifa, wanatumia utaratibu wa kura ya wazi.
Akisisitiza kwamba kwenye Bunge Maalumu wanataka msimamo, na kutoa mfano wa Bunge la Marekani, ambamo wakati wanataka kumtoa Clinton (Rais Bill), kila mtu alionesha msimamo wake wazi.  Alitaka wanasiasa kutoingiza siasa ndani ya Bunge Maalumu.
Christopher ole Sendeka, aliunga mkono kura ya wazi akisema anachoamua lazima akiseme hadharani bila kujali chama chake cha siasa, isipokuwa kwa maslahi ya wananchi na Taifa.
Sendeka alisema pia vipo vyama vinakutana na kuweka msimamo. Alitaka vyama vyenye mapendekezo, vijenge ushawishi na endapo hoja zao zitakuwa na nguvu, wataungwa mkono.
Deo Sanga, alihoji iweje itumike kura ya siri wakati suala hilo si la uchaguzi wa mtu bali ni uamuzi kwa maslahi ya wananchi na Taifa.
Henry Shekifu, alisema ni vema mjumbe aonwe na wananchi waliomtuma wabaini kama amewasaliti au la.
Salmin Awadh Salmin, alisema ni vema kura ziwe za wazi ili wananchi wawasikie na pia iondoe dhana  iliyojengeka, kwamba upo uchakachuaji katika kura za siri.
Wengine waliounga mkono kura ya wazi ni Paul Makonda na Dk Lucy Nkya.

No comments: