BOMOABOMOA WALIOVAMIA MAENEO YA WAZI YAANZA RASMI LEO...

Picha ya juu ya maeneo ya Ubungo, Dar es Salaam.
Bomoabomoa mpya inatarajia kuanza leo katika Jiji la Dar es Salaam  kwa watu wote waliojenga katika maeneo ya wazi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alitangaza kuanza kwa bomoa bomoa hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Tibaijuka alisema kuwa bomoa bomoa hiyo, itahusu wavamizi wa maeneo ya wazi na kuwa tayari walishataarifu wahusika kuondoka maeneo hayo.
Alisema pamoja na baadhi ya watu walikuwa wakimbeza kuwa juhudi zake za kurejesha maeneo ya wazi ni nguvu ya soda, watu hao wanatakiwa kutambua kuwa hajaisha na nguvu zake wanataziona kuanzia wiki hii.
"Nimepewa timu mpya na tumeshakubaliana jana (juzi) kuwa tunaanza bomoa bomoa. Watu walisema Profesa Tibaijuka ni nguvu ya soda, amekwisha mimi sijaisha sasa nawatangazia wiki ijayo (wiki hii) tunaanza bomoa bomoa."
Kwa mujibu wa Tibaijuka, Dar es Salaam ndiko kwenye majambazi wa ardhi, ambao wamevamia maeneo ya wazi na kujenga nyumba na kubainisha maeneo sugu kuwa ni Sinza ambako ndiyo watakayoanza nayo na kufuatiwa na Mbezi Beach.
"Tulishawawekea taarifa ya kuwataka waondoke katika maeneo ya wazi, iliyobaki ni kuvunja. Tunajua wanakimbilia mahakamani, lakini sisi tumejiandaa kitaalamu na tuna kikosi cha Polisi, tutavunja na tutakwenda mahakamani wanakokimbilia."
Tibaijuka alifafanua utaratibu wa sasa wa uvunjaji wa maeneo hayo, alisema watahakikisha kuwa wakati wavamizi hao wakizungumzia kesi mahakamani, nyumba zao zilizopo maeneo ya wazi zitakuwa zimevunjwa.
"Hapa kuna majambazi wa kupora ardhi sasa nawapa taarifa wakati wao umekwisha ukiwa na hati pandikizi, tutahakikisha numba imelala ndio tunakuja mahakamani kutoa ushahidi," alionya.
Akizungumzia tatizo la kukosa maadili kwa baadhi ya watendaji, Tibaijuka alisema ndani ya wizara yake kulikuwa na mfumo mbovu uliokuwa ukisababisha watendaji kuletewa vishawishi vingi.
Alisema mfumo huo pia uliwaweka katika mazingira ambayo mtendaji wizarani anaweza kuingizwa 'mkenge' baada ya watendaji wa halmashauri kushiriki kula rushwa na kutoa mapendekezo yanayokwenda kinyume na taaluma ya mipango miji.
"Katika kuzuia hili, tumeondoa utaratibu wa hati kusainiwa na kamishna mmoja wa ardhi, itasainiwa na watendaji kadhaa. Tumeondoa utaratibu wa uhusiano wa bosi anamteremshia kazi mtu wa chini, sasa watu wanakaa pamoja wakati wa kupitisha hati.
"Kabla ya kutoa hati, lazima ofisa mpimaji aende kujiridhisha ndio watu wakae meza moja na kuitoa hati badala ya utaratibu wa zamani mtu mmoja kujifungia ndani na kusaini hati ya ardhi," alisema.
Akizungumzia migogoro ya ardhi nchini, Tibaijuka alisema sekta ya ardhi ni ngumu na ugumu wake unaonekana pale mambo yanapokwenda kinyume na matarajio.
Alifafanua kuwa asilimia 80 ya malalamiko ya sekta hiyo kwa wizara yake, yako nje ya uwezo wa wizara kwa kuwa watendaji wa ardhi wako katika halmashauri zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema matatizo mengi yako huko na uwezo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kusimamia changamoto za halmashauri kitaalamu ni mdogo.
Kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji, alifafanua kuwa hali ikifikia katika mapigano, huko ni kuvunja amani na chombo kinachohusika si Wizara hiyo, ila Wizara inaingia baada ya vyombo vya kutuliza na kurejesha amani kumaliza kazi zake.

No comments: