ZITTO KABWE AENDELEA KUWAGARAGAZA AKINA MBOWE NA WENZAKE...

Mashabiki wa Zitto Kabwe wakishangilia ushindi wa Mbunge huyo mahakamani jana.
Wafuasi wanaounga mkono uongozi wa Chadema chini ya Mwenyekiti Freeman Mbowe, jana waliondoka mahakamani kwa huzuni, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuamuru Kamati Kuu ya Chadema kutojadili uanachama wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Uamuzi wa Jaji John Utamwa, ndio uliowahuzunisha wafuasi hao baada ya kukubali kwamba hoja za upande wa Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, zimekidhi matakwa ya kisheria ya kutolewa kwa zuio la muda la kutojadiliwa kwa uanachama wake.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Utamwa alisema Kamati Kuu ya chama hicho au chombo chochote cha Chadema, hakitaruhusiwa kujadili suala la uanachama wa Zitto hadi kesi yake ya msingi aliyoifungua mahakamani itakaposikilizwa.
Zitto amefungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Dk Wilibrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio hilo, hadi atakapokata rufaa ya kupinga uamuzi uliomvua uongozi wa chama.
Aidha anaiomba Mahakama imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema, Dk   Slaa ampe nakala zinazotoa sababu za uamuzi wa kumvua uongozi katika kikao kilichofanyika Novemba 22 mwaka jana, ili akate rufaa katika Baraza Kuu la Chama.
Katika uamuzi wake Jaji Utamwa alisema kwa mujibu wa Sheria ili Mahakama itoe zuio, ni lazima katika suala la msingi kuwe na mtu ambaye atapata madhara ambayo hayatarekebishika.
Alisema katika ombi la Zitto, amekidhi matakwa ya kisheria, kwa kuwa zuio hilo lisipotolewa na akavuliwa uanachama, atapoteza nafasi ya ubunge na kushindwa kuwatumikia wananchi waliomchagua na pia atapoteza nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Kudumu ya  Hesabu za Serikali.
Jaji Utamwa alisema endapo Zitto atavuliwa uanachama kabla hajapewa haki ya kusikilizwa, atapata madhara makubwa ambayo hayarekebishiki hata kama uchaguzi utafanyika tena.
Aliongeza kuwa uchaguzi ni mchakato mkubwa, unahitaji gharama na utawahusisha watu wengi wakiwemo wananchi wa jimbo lake.
Aidha alikubali hoja ya Zitto kuwa, haizuii Chadema kutekeleza majukumu yake isipokuwa kutojadili suala la uanachama wake hadi atapowasilisha rufaa yake katika Baraza la Kuu la Chama.
Awali kabla ya kutoa uamuzi huo, Jaji Utamwa alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani iliyoapwa na Wakili wa Chadema, Peter Kibatala kwa niaba ya walalamikiwa kwa kuwa ilikuwa na upungufu wa kisheria.
Alisema kwa mujibu wa Sheria, wakili anaruhusiwa kuapa kwa niaba ya walalamikaji lakini katika mazingira ya kesi hiyo, hairuhusiwi, na kutokana na jambo hilo, ombi la Zitto limebaki bila kupingwa.
Jaji Utamwa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 13 mwaka huu kesi ya msingi itakapotajwa.
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa Zitto, Albert Msando alisema uamuzi wa Mahakama umetoa nafasi kwa Zitto kusikilizwa katika jambo analolilalamikia.
Hivi karibuni Mahakama iliamuru Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wa Zitto katika mkutano uliofanyika Ijumaa iliyopita baada ya kutupilia mbali pingamizi la Chadema na kukubali ombi la Zitto.
Zitto alivuliwa wadhifa wake Chadema, sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa kilichodaiwa ni usaliti kwa chama hicho cha upinzani.
Baada ya kuvuliwa wadhifa, viongozi wa Chadema, Mbowe, Dk Slaa, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na viongozi wengine wa chama hicho, walianza ziara zilizoitwa za kuimarisha chama mikoani.
Katika ziara hizo, kauli za kuunga mkono uamuzi wa kumvua wadhifa Zitto zilitolewa na nyingine zilionesha kuwa hatua iliyokuwa ifuate ilikuwa kumvua uanachama.
Baada ya ziara hizo, Kamati Kuu ya Chadema ilipokutana Dar es Salaam, Dk Mkumbo na Mwigamba walivuliwa uanachama huku Lissu akitoa kauli kuwa Zitto uanachama wake ni wa mahakamani.
Nje ya Mahakama, Zitto aliwasili akiwa na walinzi pande zote na kupokewa na kelele za wanachama wafuasi wa akina Mbowe,  waliomuimbia wimbo wa CCMÉ CCMÉ CCM.. na kuanza kumzonga hadi akavukwa na kiatu kimoja.
Alipoingia ndani ya Mahakama, hali iliendelea kuwa shwari huku wafuasi wa akina Mbowe wakiendelea kuimba nyimbo za kumuelezea Zitto kuwa msaliti kwa chama chao.
Ilipotimu saa 7:15 kundi la wafuasi wa Zitto liliingia katika maeneo ya Mahakama kwa ngoma ya mdundiko na kuimba nyimbo za kumsifu Zitto, huku wakicheza na kuzunguka maeneo ya upande wa pili wa barabara ya Kivukoni hadi karibu ya wafuasi wa akina Mbowe.
Ilipotimu saa 7:56 hali katika maeneo hayo ilibadilika na na wafuasi wa pande zote mbili walianza kurushiana mawe yaliyopo barabara hiyo inayojengwa.
Vita ya mawe iliendelea kwa muda wa dakika kumi hivi huku kila kundi   likiwa upande wake; lile la Zitto upande wa kuelekea Posta ya Zamani na la akina Mbowe likiwa upande wa Kivukoni.
Polisi waliokuwa wamejiandaa wakiwa na magari mawili ya kuwasha na magari matatu ya aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up, yaliyokuwa na askari wa kutuliza ghasia.
Askari hao walibaki kuwaangalia na baadaye kuamua kuwafuata na kuwazuia kisha walifunga kamba maalum kwa ajili ya kutenganisha maeneo ya kukaa makundi hayo.
Katika tukio hilo, watu wawili walijeruhiwa na mawe kutoka kundi la wafuasi wa akina Mbowe akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Kata ya Gongo la Mboto, Theophil Luoga  aliyejeruhiwa kichwani na kukimbizwa katika kituo cha Polisi kwa kutumia pikipiki ya chama hicho yenye namba za usajili T. 254 CRG na kisha hospitalini.
Ilipotimia saa 11:12 taarifa za kumalizika kwa kesi ndani ya Mahakama zilianza kusikika na makundi ya pande zote mbili yalinyamaza kimya  kusikiliza uamuzi uliotolewa.
Mara baada ya kusikia kwamba  Zitto kashinda, kundi la wafuasi wake walianza kuimba, kucheza na kushangilia na baadaye kuondoka wakiimba mara baada ya Polisi kutangaza kuwa kesi imeisha na watu wote wanatakiwa kuondoka mahakamani hapo.
Wakati hayo yakiendelea, kundi lingine la chama lilikuwa kimya na kumtaka Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kufika eneo walilokuwa kuwapa taarifa.
Baada ya muda kidogo, Lissu alifika katika eneo hilo na kuwasihi wafuasi hao kuwa watulivu huku akieleza kuwa ubunge wa Zitto ni wa Mahakama na kesi bado inaendelea.
Aliwaomba wafuasi hao kuondoka kimya bila kufanya vurugu kwani hawahitaji mtu kuumia wakati walifika kusikiliza kesi ya chama, wakatii na kuondoka kwa kupitia upande wao ili wasikutane na kundi la Zitto ambalo tayari lilikuwa limeondoka.

No comments: