Christine Lagarde. |
Akihutubia Jumuiya ya Sekta Binafsi nchini Kenya juzi, mkuu huyo wa IMF alisema hadhani kwamba EAC iko tayari kwa utekelezaji wa mpango huo na inahitaji kwanza kushughulikia masuala muhimu ndani ya nchi zao kabla ya kuunganisha fedha zao, kwa mujibu wa habari zilizorushwa na Radio Capital FM ya Kenya.
Lagarde aliwasili Kenya Jumapili kwa ziara ya siku tatu kujadili uhusiano kati ya IMF na Kenya kwa kukutana na wadau mbalimbali.
Nchi wanachama wa EAC imeshaanza kutekeleza itafaki za Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja na bado hawajaanza kuonja matunda ya hatua hiyo. Hatua ya tatu ni ya Umoja wa Fedha na ya nne na ya mwisho ni Shirikisho la Kisiasa.
Miongoni mwa changamoto ambazo mkuu huyo wa IMF alizitaja ni pamoja na kuongezeka kwa vikwazo visivyo vya kodi, tofauti ya uchumi miongoni mwa nchi wanachama na tofauti za kodi ndani ya nchi hizo.
"Nikiwa mjumbe wa Umoja wa Fedha wa Ulaya, ninawajibika kuwaeleza kuwa huu ni mradi wenye kuleta hamasa sana, lakini ni mradi ambao Aristotle (mwanafalsafa wa Ugiriki) alipata kusema unatakiwa kutekelezwa kwa taratibu. Msiharakishe," Lagarde alinukuliwa na Capital Radio akisema.
Alisema Kenya ikiwa mstari wa mbele kupigia debe mtangamano wa kiuchumi, inatakiwa pia kuongoza wanachama wenzake wa Jumuiya hiyo kuhakikisha makosa yaliyofanywa na jumuiya kama hizo katika umoja kama huo, hayarudiwi. Rais Uhuru Kenyatta ndiye Mwenyekiti wa sasa wa EAC.
"Hakikisheni mnajifunza kutokana na makosa yetu na Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki unaweza pia kuwa funzo kwa ule wa Ulaya juu ya kuutekeleza kwa njia sahihi," Lagarde alisisitiza.
Itifaki ya Umoja wa Forodha wa EAC ilisainiwa na wakuu wa nchi wanachama mwezi uliopita mjini Kampala, Uganda, ukiwa umeanzisha rasmi mchakato wa kuwa na sarafu moja katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
"Kuna uzoefu mwingi, uwe wa Umoja wa Fedha wa Ulaya, Umoja wa Visiwa vya Caribbean, Umoja wa Afrika Magharibi na umoja mwingine mahali kwingine duniani. Yapo makosa, mapengo, upungufu ambavyo vinaweza kutumika kujifunza," alisema.
Sarafu moja inalenga kuboresha biashara katika eneo hili la Afrika na pia kuimarisha ushirikiano uliopo.
"Utangamano umefungua masoko mapya, umesaidia kuanzishwa kwa wafanyabiashara wa kati, na kuwezesha mahitaji ya ndani kuwa chachu ya maendeleo. Mchakato huo unapaswa sasa kuimarishwa," alielezea.
Wakati huo huo, aliitaka Kenya kuja na sera nzuri ambazo zitawezesha utekelezaji mzuri wa mabadiliko ambayo alisema ndiyo changamoto kubwa katika uchumi wa nchi hiyo.
Mfanyabiashara Chris Kirubi baadaye alielezea msimamo wa Lagarde juu ya Umoja wa Fedha kama ushauri ambao umekuja kwa wakati mwafaka.
"Huu ni ushauri uliokuja kwa wakati mwafaka kabisa, kutoka kwa Mkuu wa IMF. Umoja wa Fedha unapaswa kuwa kitu cha mwisho kabisa Kenya kuingia. Tusiruhusu kitu ambacho kitatugawa," Kirubi alisema kwa njia ya simu kutoka Dubai.
No comments:
Post a Comment