WAZIRI AAHIDI WATANZANIA KUSHUKA KWA KIASI KIKUBWA BEI YA UMEME...



Wakati Watanzania wengi ‘wakiugulia’ bei mpya ya umeme iliyoanza kutumika Januari mosi mwaka huu, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema maumivu hayo ni ya muda, kwani bei hiyo itashuka kwa kiasi kikubwa.

Amesisitiza kuwa, neema ya umeme kwa Watanzania inakuja na kwamba wasubiri tu kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, kabla ya mwishoni mwa mwaka kesho.
Profesa Muhongo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Wakala wa Jiolojia Tanzania iliyokuwa ikiainisha maeneo yenye madini nchini.
Alisema tatizo la umeme kwa Tanzania litakwisha baada ya bomba la gesi kukamilika ambapo pia bei ya umeme itapungua kwa kiasi kikubwa.
"Hii bei ya umeme iliyopo kwa sasa ni kwa muda tu na itashuka sana bomba la gesi likikamilika kwa sababu hata mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta nayo itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa, nataka Watanzania wakubali hivyo…" alisema.
Aliongeza kuwa, "Serikali inataka umeme mwingi utokane na gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba lisije Dar es Salaam na hao hao wanalalamika umeme bei juu, mtu yeyote ambaye anajua dunia inakwendaje hawezi kupinga kujengwa bomba la gesi."
Alisema muda si mrefu Tanzania haitategemea tena chanzo kimoja cha umeme wa maji, bali pia utakuwepo umeme wa makaa ya mawe na mabaki ya mimea.
"Miaka ijayo, chanzo kikubwa cha umeme nchini kitakuwa gesi asilia nyie mtanitukana, mtanisema sana lakini mimi nitabaki kwenye utaalamu na wala siwezi kuyumba, tatizo la umeme wa Tanzania litatatuliwa na gesi kama bei ya umeme itashuka…kila kitu kikikamilika Tanesco na Ewura hawawezi kuendelea kuweka bei ya juu," alisema.
Hivi karibuni pamekuwepo na malalamiko ya wengi kutokana na kupanda kwa bei ya umeme na hivyo kuongeza ugumu wa maisha miongoni mwa jamii.
Kuanzia Januari mosi mwaka huu, Tanesco imeanza kutoza bei mpya iliyoadhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ambayo inaonesha kuwa, watumiaji umeme wa majumbani watanunua uniti moja ya umeme kwa Sh 306 kutoka Sh 221 za awali.
Wateja wengi wa Tanesco wanaangukia katika kundi hili ambalo linajulikana wateja wa kundi la T-1. Katika kundi hilo ongezeko la bei kwa uniti moja ni Sh 85.
Kundi hilo ni la wateja ambao wanatumia vifaa kama majokofu, televisheni, kupiga pasi pamoja na wafanyabiashara wadogo kama wasusi, vinyozi, maduka, mashine za kusagisha na biashara zingine ndogo zinazotumia umeme.
Katika kundi hilo tozo la kutoa huduma ambayo pia anatozwa mwananchi imeongezeka kutoka Sh 3,841 hadi Sh 5,520 kwa mwezi.
Kiasi hicho mteja wa Tanesco anakilipa bila kujali kama ametumia umeme au la kwa mwezi.
Kwa upande wa watumiaji wa majumbani wadogo ambao wamekuwa wakitumia kati ya uniti sifuri hadi 50 ambao wengi wao wanaishi vijijini, wanalazimika kununua uniti moja kwa Sh 100 badala ya Sh 60 za sasa. Katika kundi hilo Ewura imeongeza wigo kuwa sasa kikomo cha watumiaji ni hadi wateja wanaotumia uniti 75 kutoka uniti 50.
Katika kundi hilo ambalo linajulikana kama D-1 mtumiaji ambaye anavuka matumizi ya uniti 75 kwa mwezi, analazimika kununua uniti moja ya umeme kwa Sh 350 badala ya Sh 275 za awali. Katika kundi hili hakuna tozo la kutoa huduma kwa mwezi.
Katika mchanganuo kundi la tatu ni T-2 ambako uniti moja ya umeme imepanda kutoka Sh 132 hadi Sh 205. Kundi hilo ni la wateja wenye matumizi ya kawaida ambao hupimwa kwa volti 400 na matumizi ya wastani ni zaidi ya uniti 7,500 kwa mwezi. Tozo la kutoa huduma kwa mwezi limebaki Sh 14,233.
Kundi la T-3-MV ambao ni wateja waliounganishwa katika msongo wa umeme wa kati, bei ya uniti ya umeme itauzwa kwa Sh 163 kutoka Sh 118. Tozo la kutoa huduma bei yake nayo imepanda katika kundi hilo kutoka Sh 14, 233 hadi Sh 16, 769.
Wateja wakubwa ambao wameunganishwa katika msongo wa juu ikiwa ni pamoja na mashirika kama ZECO, Bulyanhulu na viwanda vya saruji kama Twiga ambao wako kundi la T-3-H, wananunua uniti moja kwa Sh 159 kutoka Sh 106 za awali. Kundi hilo halitozwi tozo ya kutoa huduma.
Gharama za kuunganisha wateja ndani ya meta 30 mijini ni Sh 272,000, vijijini Sh 150,000 na kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni Sh 99,000. Umbali usiozidi meta 70 ambayo mteja ataweka nguzo moja, bei kwa mijini ni Sh 436,964, vijijini Sh 286,220 na umbali usiozidi meta 120 mijini ni Sh 590,398 na vijijini itakuwa Sh 385,300. Ada ya maombi ni Sh 5,000.

No comments: