Dk Anatory Amani. |
Meya wa Manispaa ya
Bukoba, Dk Anatory Amani amejiuzulu wadhifa huo baada ya kuguswa na taarifa ya
ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amefanya hatua hiyo
baada ya kushauriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyemtaka apime mwenyewe ama
kwa kujiuzulu au asubiri kupigiwa kura na Baraza la Madiwani za kutokuwa na
imani naye.
Taarifa ya ukaguzi wa
CAG uliofanyika kwa siku 35, ilitolewa ikionesha tuhuma zaidi ya 30 zilimgusa
Meya huyo na baadhi ya watendaji wa Manispaa hiyo akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi
wa Manispaa hiyo, Hamisi Kaputa.
“Nimeafiki na kukubali
maamuzi na maelekezo yaliyotolewa na Serikali mimi ni mtu mzima nimejiuzulu,”
alitamka amani kwa ufupi.
Taarifa ya ushauri
kutoka kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilitolewa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Serikali za Mitaa Tawala za Mikoa (TAMISEMI), Aggrey
Mwanri wakati wa kikao kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Kagera, mjini hapa.
Alisema baada ya
kuonekana kuna tuhuma za makosa mengi ya kiutendaji ikiwemo matumizi mabaya ya fedha ya umma, kusaini
mikataba kinyume bila kuwashirikisha baraza la madiwani na kuikosesha mapato
Manispaa, Serikali imeamua kutoa maagizo ya kumtaka `ajipime’.
Aidha, Mwanri alisema
Waziri Mkuu ameagiza Kiputa ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya Momba mkoani Mbeya, avuliwe madaraka mara moja.
Alisema wengine
wanaopaswa kuvuliwa madaraka mara moja ni Mhandisi wa Manispaa ya Bukoba,
Steven Nzihirwa, Ofisa Manunuzi wa Manispaa, Baraka Marwa na Mweka Hazina wa
Manispaa, Hamduni Ulomi ambaye kwa sasa inadaiwa yuko masomoni nje ya mkoa wa
Kagera.
Pia imeagizwa kuwa,
kitengo cha ukaguzi wa ndani katika Halmashauri hiyo kiimarishwe ili kiweze
kufanya kazi ipasavyo na pia itaundwa
kamati ambayo itashirikiana na Serikali za mitaa kufanya wa ukaguzi wa mambo
mengine ambayo yamebainika kuhitaji ukaguzi zaidi kikiwemo uuzwaji wa kiwanja
cha michezo cha shule ya msingi
Kiteyagwa.
Maagizo yote hayo
yametakiwa kutekelezwa ndani ya wiki moja na taarifa yake kufika Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Baadhi ya miradi iliyoibua utata na hata
kusababisha ukaguzi wa CAG na hatimaye kumng’oa meya ni ujenzi wa kituo cha
mabasi Kyakailabwa, mradi wa viwanja 5000 na viwanja 800, mradiwa ujenzi wa
kituo cha kuoshea magari cha machinjioni. Aidha, Meya anatuhumiwa kusaini mkopo
wa Sh mil. 200 bila kufuata utaratibu na kutofuata taratibu wa kuwapata
wakandarasi na kuutowashirikisha madiwani wa manispaa hiyo.
No comments:
Post a Comment