Moja ya vituo vya kuuzia umeme. |
Wafanyabiashara hao; wenye mitambo ya kufua umeme wa mafuta na waagizaji wa mafuta, wananufaika kwa kunyonya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo linalazimika kuwapa karibu Sh bilioni nne kila siku, ili lipate umeme huo wa mafuta kutoka kwao.
Akizungumza juzi katika siku ya mwisho ya ziara yake ya kutembelea ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kuchakata gesi Mtwara na Lindi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema wafanyabiashara hao wanauzia Tanesco umeme uniti moja kwa kati ya senti 33 na 50 ya dola ya Marekani.
Bei hiyo ya umeme kwa Tanesco ni kubwa kuliko ambayo shirika hilo linauza kwa wateja wanaotumia umeme mdogo wa majumbani, wa kati kwa wafanyabiashara, wa kati viwandani na mkubwa kwa viwanda vikubwa, na kubwa kuliko bei ya umeme ya mashirika ya umeme ya nchi za Afrika Mashariki.
Tanzania kwa sasa inatumia megawati 1,850 ambazo asilimia 80 kwa mujibu wa Pinda, zinazalishwa kwa mafuta ya dizeli na mazito; wakati asilimia nyingine ndizo zinazotokana na vyanzo vingine vya maji na gesi ya Songosongo.
Kwa mujibu wa takwimu za Tanesco, wateja majumbani wananunua uniti moja kwa senti 19 ya dola, wateja wa biashara senti 13 na viwanda vya kati na vikubwa senti 10. Umeme wa taa za barabarani ni senti 19.
Kwa nchi za Afrika Mashariki, hasa Kenya, Uganda na Rwanda, wateja majumbani hununua uniti moja kwa senti 20, wa biashara ni kati ya senti 16 na 20. Viwanda vya kati Uganda bei ni senti 17, Kenya 14 na Rwanda 19.
Kwa umeme wa viwanda vikubwa, bei kwa Uganda ni senti 12, Kenya 15 na Rwanda 19. Tanzania inaongoza kwa kutoza bei kubwa kwa taa za barabarani ambayo ni senti 19 sawa na Rwanda huku Kenya na Uganda bei kwa umeme huo ni senti 18.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa pamoja na kupandisha bei ya umeme mwezi huu, bado gharama za umeme kwa Tanesco ni kubwa kuliko bei ya kuuzia, na kusababisha shirika hilo muhimu katika uchumi wa nchi, kujiendesha kwa hasara.
Pinda alisema bomba la gesi kutoka Mtwara likimalizika kujengwa na uzalishaji kuanza, Tanesco itanunua umeme huo kwa senti 8 na kufanya nishati hiyo kushuka bei.
Kauli hiyo ya kushusha bei ya umeme baada ya gesi kuanza kutumika Dar es Salaam, pia ilipata kutolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
"Hii bei ya umeme iliyopo sasa ni ya muda tu na itashuka sana bomba la gesi litakapokamilika, kwa sababu hata mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta nayo itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa, nataka Watanzania wakubali hivyo.
"Serikali inataka umeme mwingi utokane na gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba kuja Dar es Salaam na hao hao wanalalamika umeme kuwa juu, mtu yeyote ambaye anajua dunia inakwendaje, hawezi kupinga kujengwa bomba la gesi.
"Miaka ijayo, chanzo kikubwa cha umeme nchini kitakuwa gesi asilia nyie mtanitukana, mtanisema sana, lakini mimi nitabaki kwenye utaalamu na wala siwezi kuyumba, tatizo la umeme wa Tanzania litatatuliwa na gesi, kila kitu kikikamilika Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) hawawezi kuendelea kuweka bei juu," alisema Profesa Muhongo.
"Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na gharama hizi ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang'anywa tonge midomoni, vita hii tunaijua; lakini hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tusonge mbele," alisema Pinda.
Alisema nyuma ya mapambano ya kuzuia gesi kufika Dar es Salaam, wapo wafanyabiashara ambao wanahofia kuwa mwisho wa biashara yao ya kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu umefika.
Alisema watu kwa sasa wananufaika na Tanesco kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme.
Katika hali hiyo, Pinda alisema uamuzi wa Serikali kuchimba gesi hiyo na kuisafirisha hadi Dar es Salaam si jambo jepesi, kwani utekelezaji wake unakabiliwa na mapambano na upinzani mkubwa kutoka kwa wenye mitambo ya kuzalisha umeme ambao kwa sasa wananufaika kutoka Tanesco.
Alisisitiza, kuwa Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta na kama wafanyabiashara hao wanataka kuendelea na biashara hiyo, ni vema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na si ya mafuta kama ilivyo sasa.
Pia alisema vita nyingine wanayokabiliana nayo ni ya nchi ambako kampuni za utafiti wa mafuta na gesi zinatoka, ambazo zinataka kampuni zao zipewe zabuni ya kutandaza bomba la gesi na kujenga mitambo ya kuchakata gesi.
"Wanalalamika gesi wametafuta na kugundua wao, halafu kandarasi anapewa China, sisi tumewajibu kuwa tumekimbilia China kwa sababu masharti yao ni nafuu kuliko yao," alisema Pinda.
Katika hatua nyingine, Pinda alitaka wakazi wa Lindi na Mtwara kutambua kuwa gesi hiyo ni rasilimali ya Taifa na itanufaisha nchi nzima.
Aliwataka wajiandae kwa uchumi huo kwa kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kufaidika.
Aliwataka wasikubali fursa ya gesi ilete balaa nchini badala ya neema. "Kama tunataka iwe neema tushirikiane na wadau wakubwa zaidi ili nchi yetu ipige hatua kimaendeleo."
Kwa upande wake, Profesa Muhongo aliwataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kusomesha watoto wao hasa katika Sayansi, ili wafaidike na uwepo wa gesi na mafuta katika mikoa hiyo.
Alisema Serikali imejitahidi kusomesha vijana katika
eneo la gesi na wamekuwa wanahamasisha vijana wa mikoa hiyo kuchukua masomo ya Sayansi kwa vile wizara inagharimia baadhi ya vijana kusoma masuala ya gesi vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.
Pinda katika ziara hiyo alielezea kuridhika na kazi inayoendelea katika mradi huo na akasema upo uwezekano mradi huo ukakamilika kabla ya muda wake uliopangwa wa miezi 18.
No comments:
Post a Comment