JWTZ KUJENGA KAMBI YA MUDA KILOSA...

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Omar Chambo (kushoto) na Mnadhimu wa Jeshi, Abdulrahman Shimbo wakikagua ukarabati wa reli baada ya kuharibiwa na mafuriko Kilosa.
Rais Jakaya Kikwete, ameagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kujenga kambi ya muda ya mahema na mabati katika kijiji cha Magole mkoani Morogoro, ili waathirika wote wa mafuriko wasio na nyumba, waishi kwenye kambi hiyo.

Mbali na agizo hilo, pia ameitaka Serikali kuandaa utaratibu wa kupata magodoro kutoka katika kampuni zinazotengeneza magodoro hayo na kuwagawia waathirika hao.
Ametoa maagizo hayo jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari Magole, ambako kumewekwa kambi ya muda kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea Januari 22, mwaka huu.
Akiwa katika kambi hiyo, Rais Kikwete aliyewasili jana mchana  kwa helkopta ya Polisi, alishuhudia idadi kubwa ya waathirika waliokumbwa na mafuriko wakiwemo watoto wadogo, wakilala chini na kuwa hatarini kupatwa na magonjwa ya vichomi na kuhara.
Kabla ya kutembelea waathirika na kuwahutubia, Rais Kikwete alitembelea daraja lililoathirika na mafuriko,  maeneo yaliyoathirika vibaya na kupewa taarifa ya athari ya mafuriko kwa kata za Wilaya ya Kilosa, Gairo na Mvomero.
"Mafuriko haya ni makubwa na hayajawahi kutokea , watu wameathiriwa kwa nyumba zao kubomoka, kujaa maji na kuwafanya kukosa makazi na wengi wao wanalala chini.
"Serikali itatafuta magodoro kati ya siku mbili hizi na kuyaleta hapa kwa waathirika wa mafuriko ili kila mmoja  alale kwenye godoro na si chini, lengo ni kuwaepusha kupatwa na magonjwa hasa ya vichomi na kwa watoto kuhara.
"Wenye viwanda hivi vya magodogo waendelee kuzalisha kwa wingi na waliyokuwa nayo stoo walete hatuwezi kuwaacha watu waendelee kulala chini," alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wa chakula, alisema Serikali inacho cha kutosha kwenye maghala yake ambayo aliagiza yafunguliwe na chakula hususani maharage na mahindi, yasambazwe kwa waathirika. Aliomba pia wadau wengine waendelee kujitokeza kusaidia kutoa chakula hasa mchele.
Kuhusu huduma ya maji, alisema itaendelea kutolewa na magari ya JWTZ, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na magari ya kampuni za ujenzi za China hadi huduma ya maji kwenye kijiji hicho na vingine itakapotengemaa.
Pia alizungumzia umuhimu wa kuwatafutia waathirika na wakazi wengine, maeneo mengine ya miiinuko yenye usalama kwa kujenga makazi yao ya kudumu.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewataka wakuu wa wilaya za Mkoa wa Morogoro pamoja na wakurugenzi watendaji wa halmashauri, kuwahudumia wananchi nyakati za matatizo, kwani uongozi wao utapimwa na wananchi kutokana na ushiriki wao wa moja kwa moja kwao.
Ametoa kauli hiyo, baada ya kutoridhishwa na takwimu za waathirika wa mafuriko zilizotolewa na uongozi wa Mkoa, kuhusu idadi ya kaya na watu waliokumbwa na mafuriko katika tarafa ya Magole, Wilaya ya Kilosa; Dakawa Wilaya ya Mvomero na Gairo kutoonesha mchanganuo halisia.
Kutokana na kasoro hizo, Rais alitoa siku moja ya jana kwa wakuu wa wilaya hizo na uongozi wa mkoa, wampatie takwimu kamili zikiwa na majina ya watu waliobomolewa nyumba ambao wanaishi kwa majirani na kambini, ili misaada inayotolewa iwafikie walengwa na si wajanja wachache ambao si walengwa.
"Uongozi unapimwa katika kipindi cha matatizo ya watu,  sijaridhika na takwimu hizi, hazioneshi walengwa halisia... jipangeni vizuri mnipe taarifa kamili kesho (leo),  ili Waziri William Lukuvi (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge) na wengine wazifanyie kazi kuwezesha upatikanaji wa huduma bila kuachwa mtu aliyeathiriwa na mafuriko," alisisitiza.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alisema  watu 12,472 walikumbwa na mafuriko hayo na kaya 2,759 zimeathiriwa, wakati nyumba 1,141 zilibomolewa na nyingine 2,922 kuzungukwa na maji.
Alisema kuna mahitaji ya tani 635.5 za chakula kwa miezi sita kuanzia sasa na Sh milioni 57 kwa ajili ya kujenga makazi ya muda.

No comments: